MAUZO YA VIWANDANI YAFIKIA SHILINGI BILIONI 66, UCHUMI WAKUA HADI ASILIMIA 6.3




Serikali imeeleza kuwa mauzo ya bidhaa za viwandani nje ya nchi yameongezeka kwa kiwango kikubwa na kufikia Dola za Marekani 25,290,157 sawa na Shilingi bilioni 66, kutoka Shilingi bilioni 29.7 zilizokuwepo mwaka 2019, huku ukuaji wa uchumi ukifikia asilimia 6.3 mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 5.2 ya mwaka 2021. 

Takwimu hizo zimetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana.

Alibainisha kuwa ongezeko hilo limetokana na kuongezeka kwa idadi ya viwanda nchini kufikia 54,084 na kutoa ajira za viwandani 454,546, jambo linaloiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotajwa kuwa na uchumi unaokua vizuri zaidi barani Afrika kupitia ushirikiano imara wa kibiashara uliowezesha biashara ya kikanda kufikia Dola za Marekani bilioni tano na biashara ya kimataifa kufikia Dola za Marekani bilioni 8.7 mwaka 2026.

Sambamba na hilo, Msigwa alieleza kuwa kupitia Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), serikali ilisajili miradi 915 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 10.9 mwaka 2025, wakati katika upande wa miundombinu ya utawala, Serikali ya Awamu ya Sita imekamilisha ujenzi wa majengo ya kudumu ya wizara zote katika Mji wa Serikali Mtumba ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan hapo kesho, Oktoba 30, 2026, ukiwa ni mji bora na unaovutia zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutokana na kujengwa kisasa na kuwa katikati ya nchi kijiografia ili kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi wote, huku kukiwa tayari na mpango wa kuanzisha gridi ya taifa ya maji kupitia Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa ili kusambaza maji maeneo ya ndani ya nchi.

Katika sekta ya nishati, Msigwa alibainisha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kutoka kuzalisha megawati 17 na 67 pekee mwaka 1961 hadi kufikia uzalishaji wa sasa wa megawati 4,646 huku Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) pekee likichangia megawati 2,115 sawa na asilimia 45 ya umeme wote nchini, na kwamba serikali imefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji vyote 12,318 nchini kwa asilimia 100 huku ikilenga kufikisha uwezo wa uzalishaji wa megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Aidha katika uendelezaji wa miundombinu ya barabara na usafiri, serikali imejenga kilometa 2,018 za barabara za lami na inaendelea kukamilisha kilometa nyingine 2,550, kujenga madaraja makubwa tisa yakiwemo Daraja la Tanzanite na Daraja la Magufuli Kigongo–Busisi, pamoja na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege tisa mikoani na Jengo la Abiria la Terminal III katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Ukuaji huo wa kiuchumi na kijamii umeenda sambamba na ongezeko kubwa la uzalishaji wa mazao ya chakula ambapo mahindi yalifikia tani milioni 10 katika msimu wa 2024/2025 kutoka tani milioni saba za mwaka 2021, wakati mchele ulifikia tani milioni 2.6, mafanikio yaliyochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha umasikini nchini kupitia afua mbalimbali za serikali, ambapo umasikini wa mahitaji ya msingi umepungua kutoka asilimia 38.6 mwaka 1991/1992 hadi asilimia 25.1 mwaka 2025, wakati umasikini wa chakula umepungua kutoka asilimia 22 hadi asilimia 8.3 na pengo la umasikini likishuka hadi kufikia asilimia 6.3.

No comments