Maandalizi ya mishahara mipya Zanzibar imefikia asilimia 95




SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema maandalizi ya mishahara mipya ambayo inatarajiwa kulipwa kwa wafanyakazi wa serikali kuanzia mwezi huu yamefikia asilimia 95. 

Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Sheria, Katiba, Utumishi na Utawala Bora, Omar Haji Gora wakati akifungua mafunzo yaliyowajumuisha wakurugenzi wa utumishi serikalini pamoja na maofisa wanaoshughulikia utumishi na mipango katika Chuo cha Utalii Maruhubi Unguja. 

Alisema ahadi ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi aliyoitoa katika kilele cha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) mwaka jana imetekelezwa ambapo mishahara mipya inatarajiwa kuanza kulipwa kwa watumishi wote kuanzia mwezi huu. 

Aiha alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwaweka katika utayari ikiwemo kujua utaratibu mzima uliotumika katika ongezeko la mishahara mipya.

Akizungumza, Mkurugenzi wa Idara ya Miundo ya Taasisi, Utumishi na Maslahi ya Watumishi, Maulid Shaibu Ahmada aliwataka watumishi kuondoa wasiwasi kuhusu marekebisho hayo ambayo yamezingatia kila kada kwa mujibu wa utendaji wake.

 Alisema serikali katika mishahara mipya imezingatia masuala yanayohusu watumishi wa umma wakiwemo watumishi wapya kwa kuzingatia kanuni zinazosimamia masuala ya utumishi. 

“Malipo ya watumishi wa umma huzingatia nafasi na majukumu ya kila mmoja huku marekebisho ya miundo ya kada yakiendelea kusimamiwa kwa kuzingatia sheria kanuni na maelekezo ya idara ya utumishi,” alisema.

 Baadhi ya maofisa utumishi waliohudhuria mafunzo hayo waliahidi kuyetekeleza ikiwemo kusimamia wafanyakazi wao kuona wanapatiwa maelekezo ya kina kuhusu marekebisho ya mishahara mipya. 

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika kilele cha sherehe za siku ya wafanyakazi Dunia Mei Mosi, mwaka jana aliahidi mishahara mipya kwa wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kima cha chini kitakuwa Sh 500,000 kutoka Sh 300,000 na kuanza kulipwa mwezi huu.

No comments