WAZIRI KIJAJI AKAGUA MIRADI YA UTALII PUGU-KAZIMZUMBWI KWA MAANDALIZI YA AFCON
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), amekagua maendeleo ya miradi ya utalii ikolojia katika Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia ya Pugu-Kazimzumbwi, inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), iliyopo Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, leo Oktoba 20, 2026.
Miradi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kwa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), inayowezeshwa kupitia Tozo ya Maendeleo ya Utalii (Tourism Development Levy – TDL), kwa lengo la kuboresha miundombinu na huduma za utalii na kuongeza uwezo wa kupokea wageni.
Katika ziara hiyo, Waziri Kijaji amekagua ujenzi wa cottages na miundombinu saidizi, miundombinu ya burudani pamoja na mabanda ya kupumzikia watalii katika eneo la Bwawa la Minaki. Aidha, amezungumza na watumishi wa hifadhi hiyo kuhusu utekelezaji wa shughuli za utalii ikolojia na maendeleo ya miradi inayotekelezwa.
Wakatik huo huo Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameagiza miradi inayotekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa fedha za Tozo za Maendeleo ya Utalii (TDL) katika Hifadhi ya Pande, jijini Dar es Salaam, ikamilike kabla ya Desemba 2026 ili kuimarisha huduma na kutumia fursa za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Maelekezo hayo yametolewa wakati wa ziara yake hifadhini hapo Oktoba 20, 2026 akiwa pamoja na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande (Mb) ambaye akizungumza kwa niaba ya Waziri, Mhe. Chande ameipongeza TAWA na kueleza kuwa Wizara imeridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tunataka ifikapo Desemba 2026 miradi hii iwe imekamilika, na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iwe imeanza kuitangaza na kuipeleka sokoni. Msisitizo wetu ni kuunganisha utangazaji na mauzo ili juhudi za kuitangaza miradi hii zilete wageni na kuongeza mapato,” amesema Mhe. Chande.
Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, amesema ujenzi wa bwawa la kuogelea na viwanja vya michezo unalenga kukidhi mahitaji ya wageni, hususan wanafunzi wanaopendelea michezo sambamba na kutazama wanyamapori. Ameeleza kuwa miradi hiyo, yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 1.24, ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji huku baadhi ikifikia asilimia 65, 75 na 90.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji, Kamanda wa Hifadhi ya Pande, Maajabu Mbogo, amesema maboresho ya miundombinu na huduma yamechangia kuongezeka kwa watalii kutoka 224 mwaka 2020/2021 hadi 6,397 mwaka 2025/2026. Katika kipindi hicho, mapato yameongezeka kutoka shilingi milioni 3.66 hadi shilingi milioni 80.19.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha Julai–Septemba 2026, hifadhi imepokea watalii 1,925 na kukusanya shilingi milioni 30.20. Takwimu hizo ni ongezeko la asilimia 17 kwa watalii na asilimia 41 kwa mapato, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Wananchi wamehimizwa kutembelea Pande kufurahia vivutio na shughuli mbalimbali, zikiwamo kutazama wanyamapori na ndege, matembezi ya asili na kupiga kambi. Upanuzi wa huduma hizo unatarajiwa pia kuongeza fursa za ajira na masoko kwa jamii zinazozunguka hifadhi.

Post a Comment