TANTRADE YAWAHIMIZA WATANZANIA UINGEREZA KUGEUZA UHUSIANO WA NYUMBANI KUWA FURSA
Na Mwandishi Wetu, BSKY Media
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Mafuru, amewakaribisha rasmi Watanzania waishio Uingereza na maeneo jirani kushiriki katika Maonesho ya 51 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, yatakayofanyika kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 13 Julai 2027.
Mafuru ametoa wito huo wakati wa mkutano na Diaspora London Uingereza hivi karibuni.
Aliwataka washiriki kikamilifu katika maonesho hayo kama waoneshaji wa bidhaa na huduma au kwa kuambatana na wanunuzi na wawekezaji kutoka nchini Uingereza.
Akifafanua wito wake alisema kuwa fursa hiyo ya kibiashara itachochewa zaidi na kuanza kwa safari za moja kwa moja za shirika la ndege la British Airways kutoka London Gatwick kwenda Kilimanjaro na Zanzibar kuanzia tarehe 29 Mei 2027, hatua itakayorahisisha usafiri wa wafanyabiashara, watalii, na usafirishaji wa mizigo kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza katika mkutano maalum uliofanyika jijini London Hivi karibuni, ikiwa ni siku tatu tu baada ya kukamilika kwa Jukwaa la Uwekezaji la Tanzania la Mwaka 2026, Mafuru aliwahimiza Watanzania waishio Uingereza kutumia uelewa wao wa kina wa masoko ya nchi zote mbili ili kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Uingereza, kuwekeza nyumbani, na kuitangaza kwa fahari chapa ya taifa ya Made in Tanzania.
Alibainisha kuwa ingawa Diaspora wamekuwa wakituma fedha nyingi nyumbani kwa ajili ya familia zao, umefika wakati wa kugeuza uhusiano huo kuwa mfumo rasmi wa kibiashara unaoweza kuzalisha mapato endelevu ya kila mwezi badala ya kutegemea matumizi ya mara moja.
Akiwasilisha takwimu za kiuchumi, Mkurugenzi Mkuu huyo wa TanTrade alipongeza mchango mkubwa wa Diaspora, ambapo fedha walizotuma nyumbani zilifikia shilingi trilioni 3.3 katika mwaka wa fedha wa 2024 na 2025, ikiwa ni ongezeko kutoka shilingi trilioni 2.1 zilizorekodiwa mwaka uliotangulia, huku Uingereza ikiwa miongoni mwa vyanzo vitatu vikubwa vya fedha hizo.
Hata hivyo, alieleza kuwa jumla ya biashara ya bidhaa na huduma kati ya Tanzania na Uingereza ni takriban pauni milioni 697 kwa mwaka, ambapo kwa upande wa bidhaa pekee mwaka 2025, Tanzania iliuza bidhaa za dola za Marekani milioni 29 nchini Uingereza na kununua bidhaa za dola milioni 211.
Licha ya mauzo ya Tanzania kuongezeka kwa asilimia 83 mwaka 2025, takwimu za Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) zinaonyesha fursa ya ziada ya dola milioni 19.4 ambayo bado haijatumiwa, huku Mpango wa Uingereza wa Biashara kwa Nchi Zinazoendelea (DCTS) ukiruhusu asilimia 99 ya bidhaa za Tanzania kuingia nchini humo bila kulipa ushuru.
Akitumia zao la korosho kama mfano wa kuigwa, Bwana Mafuru alieleza kuwa Tanzania ilivuna rekodi ya tani 617,683 katika msimu wa 2025 na 2026, ikiwa ni bidhaa ya pili kwa ukubwa kati ya zile ambazo Tanzania inauza Uingereza.
Hata hivyo, alibainisha kuwa Uingereza huagiza tani 17,000 hadi 19,000 za korosho zilizobanguliwa kila mwaka zenye thamani ya karibu dola milioni 100, lakini takriban asilimia 91 ya korosho hizo hutoka nchini Vietnam, nchi ambayo hainulimi korosho kwa kiwango cha Tanzania.
Alisisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kubadilika kwa sababu korosho zilizobanguliwa na kufungashwa nchini Tanzania zina haki ya kuingia katika soko la Uingereza bila ushuru chini ya mpango wa DCTS, na hivyo kutoa fursa kubwa ya uwekezaji katika usindikaji na ubanguaji wa ndani.
Kutokana na fursa hizo, Mafuru alitaja njia tano kuu ambazo Watanzania waishio Uingereza wanaweza kuchangia katika kukuza uchumi wa taifa, zikijumuisha kuwa waagizaji na wasambazaji wa bidhaa za Tanzania nchini Uingereza, na kushirikiana na wasindikaji wa ndani nchini Tanzania katika mikataba ya ununuzi na usambazaji ili kukuza uzalishaji.
Njia nyingine ni kuwekeza nyumbani katika usindikaji na ufungashaji kupitia Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (TISEZA) kwa Tanzania Bara au Mamlaka ya Usimamizi wa Maeneo Huru ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), kuwa mabalozi wa chapa ya Made in Tanzania, pamoja na kuwa daraja la maarifa kwa kubadilishana taarifa za masoko, ujuzi, na mtandao wa wanunuzi.
Mkurugenzi Mkuu huyo aliwahimiza Diaspora kutumia na kusajili bidhaa zao chini ya nembo ya taifa ya Made in Tanzania – Fahari ya Tanzania iliyozinduliwa rasmi mwezi Julai 2025, pamoja na kujisajili kwenye Mfumo wa Kidijitali wa Diaspora (Diaspora Digital Hub) unaoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Post a Comment