EU yaachia bil 461/- za maendeleo Tanzania



UMOJA wa Ulaya (EU) umeidhinisha kuipatia Tanzania fedha za maendeleo Euro milioni 156 ambazo ni sawa na takribani Sh bilioni 461. EU ilisitisha programu yake kutokana na matukio ya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. 

Mkuu wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya EU nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marc Stalmans amesema Julai 23, mwaka huu Umoja huo ulifanya maamuzi ya kuendelea kutoa fedha zote zilizotengwa sanjari na kuendelea na malengo na shughuli zilizopangwa. 

Fedha hizo ni sehemu ya mpango wa ushirikiano wa EU na Tanzania 2021-2027 unaozingatia masuala ya kuendeleza rasilimaliwatu, mazingira, ajira, uongozi, miundombinu, dijiti naushirikiano kimataifa. 

Stalmans alisema Dar es Salaam fedha hizo zipo kwa ajili ya Tanzania tangu Julai 23, mwaka huu. 

Novemba mwaka jana Bunge la Ulaya liliamua kusitisha uamuzi wa pendekezo la kuipatia Tanzania fedha kutokana na matukio ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. 

Hatua hiyo imekuja wakati Marekani ikitangaza kupunguza kiwango cha tahadhari ya usafiri kwa raia wake wanaotaka kutembelea Tanzania kilichokuwa kimewekwa baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilishusha tahadhari ya usafiri kwa Tanzania kutoka kiwango cha tatu kinachowataka wasafiri kufikiria upya safari zao hadi kiwango cha pili kinachowashauri kuongeza umakini wanapokuwa nchini.

Marekani ni miongoni mwa masoko muhimu ya watalii wanaotembelea Tanzania hivyo uamuzi huo unatarajiwa kunufaisha wadau wa sekta ya utalii . 

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo Tanzania ilipokea takribani watalii wa kimataifa milioni 2.29 mwaka 2025, ikilinganishwa na milioni 2.14 mwaka 2024. 

Aidha mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kwa asilimia 13 na kufikia Dola za Marekani bilioni 4.41 mwaka 2025, kutoka Dola bilioni 3.90 mwaka uliotangulia.


No comments