WAZIRI MKUU AKEMEA VIKALI VITENDO VYA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI



 WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amekemea vikali vitendo vya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuvielekeza vyombo vya dola kuchukua hatua stahiki na kali kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi katika ngazi za vijiji na kata kuhakikisha kuwa uuzaji na ugawaji wa maeneo unazingatia miongozo ya matumizi bora ya ardhi ili kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza, ikiwemo migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Dkt. Mwigulu ametoa maagizo hayo leo, Oktoba 26, 2026, wakati akizungumza na wabunge wa Mkoa wa Ruvuma, jijini Dodoma kufuatia vurugu zilizotokea hivi karibuni baina ya wakulima na wafugaji, ambazo zimesababisha madhara mbalimbali vikiwemo vifo.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Serikali haivumilii vitendo vya uvunjifu wa sheria na amewataka wananchi kuheshimiana, kuvumiliana na kuzingatia sheria katika kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.

Amesema Serikali haiungi mkono uchukuaji wa sheria mkononi, utaratibu huo ni kinyume cha Katiba na sheria za nchi, hivyo kila mwananchi anapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na kuviachia vyombo vya dola kutekeleza wajibu wake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa pole kwa wananchi wa Wilaya ya Tunduru na Watanzania wote walioathiriwa na matukio hayo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na makosa hayo.

Kuhusu matumizi ya ardhi, Dkt. Mwigulu amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha ardhi inatumika kwa kuzingatia mipango na miongozo iliyowekwa kwa lengo la kuimarisha amani, kuzuia migogoro na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi kwa usalama.

Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda tunu za Taifa, hususan amani na mshikamano, akisisitiza kuwa tofauti za kiuchumi na matumizi ya ardhi zinapaswa kutatuliwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.

Kwa upande wao, wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wameishukuru Serikali kwa hatua inazoendelea kuchukua kukabiliana na migogoro hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa matumizi ya ardhi pamoja na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao.

No comments