Tanzania Kuwa Wenyeji wa Mkutano Mkuu wa Uhamaji wa Wafanyakazi Oktoba Mwaka Huu


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akiwa kaitika mazungumzo na Waziri wa Kazi wa Qatar, Mhe. Dkt. Ali bin Samikh Al Marri, leo Julai 8, 2026, jijini Doha, nchini Qatar.


Na Mwandishi Maalumu, Doha

Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa wa Uhamaji wa Wafanyakazi (Labour Mobility Dialogue) mwezi Oktoba 2026 jijini Dar es Salaam, utakaowakutanisha wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC), Jordan, Lebanon na nchi za Afrika zilizo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika (AU). 

Maandalizi na ajenda za mkutano huo wenye lengo la kuimarisha ushirikiano na kupanua fursa za ajira salama na zenye staha duniani zimejadiliwa kwa kina jijini Doha, Qatar, katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika leo Julai 8, 2026, kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, na Waziri wa Kazi wa Qatar, Mhe. Dkt. Ali bin Samikh Al Marri.



Kikao hicho cha ngazi ya juu kimejikita pia katika kuimarisha ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Qatar kwenye sekta ya kazi na ajira, hususan katika maeneo ya kukuza rasilimali watu, ulinzi na uhakikishaji wa haki za wafanyakazi, pamoja na kufungua milango zaidi ya ajira kwa Watanzania nchini Qatar. 

Katika kuhakikisha utekelezaji wa mikakati hiyo, Waziri Sangu aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Awesi Mohamed, Naibu Katibu Mkuu Zuhura Yunus, pamoja na viongozi waandamizi kutoka wizara za kazi na ajira za Tanzania Bara na Zanzibar.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akimkabidhi tuzo Waziri wa Kazi wa Qatar, Mhe. Dkt. Ali bin Samikh Al Marri, tuzo ya kutambua ushirikiano katika ya Tanzaniana Qatar katika masuala ya Ajira, leo Julai 8, 2026, katika Ofisi za Wizara hiyo ya Kazi Jijini Doha, nchini Qatar.



No comments