Gavana Tutuba Aanika Siri ya Tanzania Kukusanya Dhahabu ya Shilingi Trilioni 9.76




Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema mpango wa kununua dhahabu si tu kwamba umeiwezesha nchi kuhifadhi dhahabu kama mbadala wa kutunza fedha za kigeni, lakini pia umeongeza urasimishaji kwenye sekta ya madini na ujumuishi wa kifedha kwa wauza madini hayo, wakiwemo wachimbaji wadogo. 

Aidha, kutokana na mpango huo, Benki Kuu imewezesha makundi hayo kufungua zaidi ya akaunti 4,000 katika taasisi mbalimbali za fedha, hususan benki za biashara.

Bw. Tutuba aliyasema hayo wakati akishiriki mjadala kuhusu Mikakati ya Ununuzi wa Dhahabu ya Benki Kuu, ikiwa ni sehemu ya mijadala ya Mkutano wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa unaojulikana kama African Caucus 2026. Mkutano huo unaozihusisha nchi 54 za Afrika unafanyika katika Kituo cha Mikutano cha SDJK, jijini Banjul nchini Gambia.

Akizungumzia mafanikio hayo, Gavana alieleza kuwa katika kipindi cha miezi 18 iliyopita, Benki Kuu ya Tanzania imenunua na kuhifadhi takriban tani 28 za dhahabu, zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.68, ambazo ni sawa na shilingi trilioni 9.76 kwa bei ya soko. 

Hatua hiyo ni mkakati wa Serikali wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kulinda thamani ya shilingi, kuleta uthabiti wa sekta ya fedha, pamoja na kukuza ukuaji wa uchumi wa taifa.

Aliongeza kuwa kutokana na bei nzuri ya soko ambayo Benki Kuu inatoa kwa wafanyabiashara wa madini, kumekuwa na mwitikio chanya sana kutoka kwa wafanyabiashara na wachimbaji. 

Benki Kuu imekuwa ikiwalipa wachimbaji na wafanyabiashara hao kwa wakati, ndani ya saa 24 tangu kufanyika kwa mauzo, na inawalipa kwa bei ya soko la dhahabu la London la siku hiyo, jambo linalowavutia sana wadau hao kuendelea kuiuzia dhahabu taasisi hiyo.



Mkutano huo wa African Caucus ni jukwaa muhimu linalowakutanisha magavana wa Afrika katika Shirika la Fedha la Kimataifa na Kundi la Benki ya Dunia, ambalo huzisaidia nchi za Afrika kuzungumza kwa sauti moja kuhusu masuala mbalimbali kama usimamizi wa madeni, fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya miundombinu, kupunguza umasikini, kukuza ajira, biashara, na mageuzi ya kiuchumi.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar, na umewashirikisha pia Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria anayehudumia pia shughuli za kibalozi nchini Gambia, Mhe. Balozi Selestine Kakele. Mkutano huo umewakutanisha wadau wengi wakiwemo viongozi wa Afrika, watunga sera, wataalamu wa fedha, na washirika wa maendeleo kutoka nchi 54 za Bara la Afrika pamoja na wawakilishi wa taasisi za kimataifa za IMF na Benki ya Dunia.

Source: Benny Mwaipaja, Banjul, Gambia

No comments