Meja Jenerali Fadhili Omary Nondo akabidhi bendera kwa kikosi cha Ushirikiano Imara 2026




Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Meja Jenerali Fadhili Omary Nondo  amekabidhi Bendera ya Taifa kwa kikosi kitakachoshiriki operesheni ya pamoja ya kijeshi ya Ushirikiano Imara 2026  ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Kenya.

Akikabidhi bendera hiyo katika ofisi za Brigedi ya 303 Mbuni wilayani Monduli mkoani Arusha,  Meja Jenerali Nondo amewataka washiriki wa Tanzania wanaokwenda nchini Kenya  kuzingatia nidhamu, uzalendo na weledi ili kuendelea kuiwakilisha vyema Tanzania kimataifa.

Alisema washiriki wanapaswa kufuata maelekezo ya viongozi wao na kutumia mafunzo waliyopewa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa. 

Meja Jenerali Nondo alisema operesheni hiyo ya 14 ya pamoja ya vituo vya uamrishaji vya kijeshi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inalenga kuimarisha uwezo wa vikosi vya nchi wanachama kukabiliana na changamoto za usalama, kudumisha amani na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi katika ukanda wa Afrika Mashariki. 

“Tunatarajia washiriki wote kutoka Tanzania mtaonesha uwezo mkubwa, nidhamu na uzalendo ili kuendelea kuipa heshima nchi yetu,” alisema. 

Alisema operesheni hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uwezo wa vikosi vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na majanga, ugaidi, uharamia na migogoro mbalimbali ya kiusalama. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikundi cha Tanzania kinachokwenda Kenya ambaye pia ni Msimamizi Mkuu wa operesheni hiyo kwa nchi za EAC, Brigedia Jenerali Maneno Mabakila alisema shughuli hiyo itafanyika nchini Kenya kuanzia Mei 13 hadi 28, 2026. 

Alisema operesheni hiyo itahusisha washiriki 341 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia. 

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mabakila Tanzania itawakilishwa na washiriki 69, wakiwemo maofisa na askari 42 wa JWTZ, askari tisa wa Jeshi la Polisi na watumishi 18 kutoka taasisi za kiraia. Alisema washiriki hao tayari wamepatiwa mafunzo maalumu ya pamoja kuhusu operesheni za kulinda amani, kupambana na ugaidi, kudhibiti majanga na kukabiliana na uharamia.

No comments