BAJETI 2026/2027 : Wafanyabiashara Wapya Kusamehewa Kodi Mwaka Mmoja
Serikali imetangaza mkakati kabambe wa kuwainua kiuchumi vijana, wanawake, na makundi maalum nchini kupitia mabadiliko makubwa ya kisera na kisheria yaliyowekwa kwenye Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2026/27.
Lengo
kuu la mkakati huo ni kurasimisha sekta isiyo rasmi na kupunguza mzigo wa mitaji
kwa wajasiriamali wanaochipukia.
Akiwasilisha mapendekezo hayo,
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema kuwa Serikali inatoa msamaha
wa kodi ya mapato kwa mfanyabiashara yeyote mpya kwa kipindi cha mwaka mmoja
tangu anapopata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN). Hatua hii inalenga
kuwapa wafanyabiashara chipukizi muda wa kukuza biashara zao kabla ya kuanza
kuchangia kodi ya serikali.
Aidha, Serikali imefanya mapinduzi makubwa katika sheria ya ugawaji wa mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri).
Katika bajeti hii mpya, kiwango cha mapato ya ndani
kinachopaswa kutengwa kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa wanawake, vijana,
na watu wenye ulemavu kimeongezwa hadi kufikia asilimia 15 kutoka kiwango cha
awali cha asilimia 10.
"Sensa ya mwaka 2022 ilionesha kuwa theluthi mbili ya Watanzania ni watoto na vijana," alisema Balozi Omar.
"Ni wajibu wetu kujenga uchumi unaozalisha fursa zaidi za ajira na
maendeleo kwa vijana na wanawake ili kukuza ukuaji jumuishi wa uchumi nchini wetu."
Post a Comment