Maridhiano na Mazungumzo ni Nguzo ya Amani na Umoja wa Kitaifa




Hakuna njia ya mkato ya kuleta amani isipokuwa mazungumzo, hayo yamesemwa na mwanasiasa mkongwe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akisisitiza kuwa katika siasa za ulimwengu, maridhiano ndiyo njia pekee ya kufikia utulivu wa kudumu. 

Katika mahojiano maalumu na TBC, Wasira amefafanua kuwa jambo hilo linatekelezwa na serikali kupitia mpango maalumu wa 4R ulionzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku akiongeza kuwa maridhiano hayo ndiyo hatua muhimu ya kufikia lengo la kupata katiba mpya.

Wasira amebainisha kuwa maridhiano yaliyofanyika kati ya Chama cha ACT Wazalendo na CCM yataleta manufaa makubwa nchini ikiwemo kuondoa tofauti za kisiasa pamoja na kuimarisha zaidi umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi. 

Aidha, mwanasiasa huyo amesisitiza kuwa uhuru na umoja ni urithi muhimu aliouacha muasisi wa Taifa la Tanzania, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mambo ambayo yanapaswa kulindwa kwa nguvu zote na kila mwananchi.

Katika kuhitimisha msimamo wake, amefafanua kuwa licha ya Tanzania kuwa nchi yenye makabila mengi na tofauti za kisiasa, hali hiyo haipaswi kuwa sababu ya kuvunja misingi ya umoja na amani iliyoachwa na Baba wa Taifa. Amesema kuwa mazungumzo ndiyo nyenzo kuu ya kudumisha misingi hiyo ili kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kuwa na utulivu licha ya tofauti za kiitikadi zilizopo miongoni mwa wananchi wake.

No comments