MAKONDA AFUNGUA MILANGO YA BONGO MOVIE ULAYA, TANZANIA KUSHIRIKI TAMASHA LA CANNES 2027




Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amewataka wasanii wa tasnia ya filamu nchini (Bongo Movie), wakiwemo waigizaji, waandishi wa miswada ya filamu (scripts), waongozaji, waandaaji na wasambazaji wa filamu, kujiandaa kutumia fursa mpya zitakazowawezesha kuingia katika soko la kimataifa, hususan nchini Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya.

Makonda ametoa wito huo katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa baada ya kufanya mazungumzo na uongozi wa waandaaji wa Cannes International Film Festival, yakilenga kujenga ushirikiano wa kuikuza tasnia ya filamu ya Tanzania na kuiwezesha Bongo Movie kushiriki kikamilifu katika soko la filamu duniani.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Makonda alisema Serikali inalenga kufungua fursa kwa wadau wote wa tasnia ya filamu kuanzia waandishi wa miswada, waigizaji, waongozaji, waandaaji hadi wasambazaji ili kazi zao zipate nafasi katika masoko makubwa ya kimataifa.

“Tumekuwa na mazungumzo mazuri sana. Lengo letu ni kuona tasnia nzima ya filamu inanufaika kwa kuwapa fursa waandishi wa scripts, waigizaji, waandaaji na wasambazaji wa filamu kuingia katika soko la dunia. Bongo Movie ni tasnia inayowagusa na kuwaingizia kipato maelfu ya Watanzania,” alisema Makonda.

Aliongeza kuwa mafanikio yaliyowekwa na mastaa wa filamu nchini, akiwemo marehemu Steven Kanumba, Ray Kigosi, Irene Uwoya, Kajala Masanja, Aunt Ezekiel, Steve Nyerere pamoja na wengine wengi, yameitangaza Tanzania ndani ya Afrika na sasa wakati umefika wa kuitangaza zaidi katika soko la dunia.

Makonda alisema hatua ya kwanza ya ushirikiano huo ni ushiriki wa Tanzania katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Cannes litakalofanyika mwezi Mei 2027 nchini Ufaransa, ambapo tayari nafasi maalumu imehifadhiwa kwa ajili ya kuonesha kazi za wasanii wa Tanzania.

“Tamasha la Cannes ni moja ya matukio makubwa zaidi ya filamu duniani. Tayari tumefanya maandalizi ya awali na tarehe 14 Mei 2027 tutapata nafasi ya kuonesha kazi za wasanii wetu. Hapo ndipo waigizaji, waongozaji, watayarishaji na wadau wa filamu kutoka duniani kote hukutana. Tumekubaliana kuharakisha mchakato huu na kuuwasilisha kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili tupate baraka zake na kuiingiza rasmi Tanzania katika jukwaa hili la kimataifa,” alisema.

Aidha, Makonda alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa kwa wasanii wa Tanzania, akitolea mfano hatua zake za kuunganisha sekta ya sanaa ya Tanzania na Korea Kusini pamoja na mipango ya kuanzisha jumba kubwa la kisasa la maonyesho ya filamu nchini.

Aliwataka wasanii wa Bongo Movie kujiandaa kutumia fursa hiyo kwa kuongeza ubora wa kazi zao ili ziweze kushindana katika soko la kimataifa.

“Hii ni fursa kubwa kwa Bongo Movie. Tusibaki kucheza ndani ya masoko yale yale ya Afrika pekee. Tunataka kuvuka mipaka, kufika Ulaya na dunia nzima ijue ubora wa filamu za Tanzania. Tuendelee kumuombea Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kufungua milango ya fursa kwa sekta yetu ya sanaa,” alisema Makonda.

No comments