Taekwondo waandaa mashindano ya taifa



SHIRIKISHO la Taekwondo Tanzania (TTF) limetangaza kuandaa mashindano ya taifa ya Taekwondo yatakayofanyika baadaye mwaka huu Dar es Salaam, ikiwa ni moja ya jitihada za kukuza na kuendeleza mchezo huo nchini. 

Katibu Mkuu wa TTF, Joseph William alisema michuano hiyo inalenga kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika Taekwondo hasa kwa vijana japo hajasema tarehe na mwezi wa michuano hiyo .

Alieleza kuwa shirikisho hilo tayari limeanzisha programu za mafunzo ya kanda nchi nzima, ambapo wanamichezo hukusanyika mara mbili kwa mwezi kwa ajili ya mafunzo ya kuboresha ujuzi wao. 

“Tumekuwa hatufanyi kazi kwa miaka mingi, lakini uongozi mpya wa TTF umejitolea kufufua mchezo,” alisema William. 

Aliongeza: “Hivi sasa tuna mafunzo ya kanda ambapo wachezaji hukutana mara mbili kila mwezi. Pia, tunatekeleza programu za maendeleo ya vijana na mwaka huu tunapanga kuandaa michuano ya taifa Dar es Salaam”. 

Alifafanua mipango hiyo inatarajiwa kuimarisha ukuaji wa mchezo na kuvutia wafadhili kusaidia shughuli za shirikisho hilo. 

Aidha, alisema Tanzania haitapeleka wanamichezo kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola inayotarajiwa kuanza Julai 23 hadi Agosti 2, mwaka huu Glasgow, Scotland. 

Alieleza kuwa shirikisho hilo halikupokea mwaliko kutoka kwa Kamati ya Olimpiki Tanzania ambacho ni chombo cha ndani cha kuratibu michezo hiyo.


No comments