TAASISI YA IMF YAIDHINISHA TRILIONI 1.2 KWA TANZANIA KUENDELEZA MAPINDUZI YA KIUCHUMI



Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeidhinisha kutolewa mara moja kwa takriban dola za Marekani milioni 443.9, ambazo ni sawa na zaidi ya shilingi trilioni 1.2 za Kitanzania, baada ya kukamilisha tathmini za mwisho chini ya programu mbili za kimkakati. 

Fedha hizo zinalenga kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii chini ya mpango wa Extended Credit Facility (ECF) uliotengewa dola milioni 158.75, pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi chini ya mpango wa Resilience and Sustainability Facility (RSF) uliopata dola milioni 298.37. 

Uamuzi huo uliotangazwa kwenye taarifa rasmi ya shirika hilo kufuatia kukamilika kwa mapitio ya sita na saba ya ECF pamoja na mapitio ya tatu na nne ya RSF, unaashiria kuendelea kwa imani kubwa ya taasisi hiyo kwa mwenendo na usimamizi wa kiuchumi wa nchi.

Ripoti ya IMF imeonyesha kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuonyesha uimara mkubwa, huku ukuaji wa Pato la Taifa ukifikia asilimia 5.9 mwaka 2025 na kutarajiwa kushika kasi hadi kufikia karibu asilimia 6.2 kwa muda wa kati. 

Ukuaji huu unachochewa kwa kiasi kikubwa na ufanisi katika sekta za madini, kilimo, na utalii, sambamba na udumishaji wa utulivu wa uchumi mpana uliowezesha mfumuko wa bei kubaki chini ya asilimia 4.0. 

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Bo Li, ameisifu Tanzania kwa kulinda utulivu huo licha ya misukosuko ya ndani na nje, ingawa alibainisha kuwa kupanda kwa bei za mafuta duniani na kuendelea kwa mzozo wa Mashariki ya Kati kunaweza kuleta shinikizo kwenye gharama za maisha na ukuaji wa uchumi.

Katika utekelezaji wa mageuzi ya kiuchumi, IMF imeridhishwa na jinsi vigezo vingi vya utendaji vilivyofikiwa kwa wakati, ingawa ilibainisha kuchelewa kwa baadhi ya malengo katika maeneo ya nishati, usimamizi wa kodi ya VAT, utawala wa Benki Kuu, na uwekezaji wa umma. Shirika hilo limeishauri serikali kuongeza kasi katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuboresha usimamizi wa fedha za umma, na kuongeza uwekezaji kwenye huduma za kijamii kama elimu na afya ili kukabiliana na changamoto za muda mrefu za kupunguza umaskini na kuandaa fursa kwa idadi ya watu inayokua.

Akipokea maamuzi hayo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ametoa shukrani zake za dhati kwa IMF kwa kuendelea kuamini na kuunga mkono mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo nchi inapiga hatua hadi sasa. Ushirikiano huu wa kihistoria kati ya Tanzania na IMF ulioanza tangu tarehe 10 Septemba 1962, umeshuhudia jumla ya ahadi za mikopo na misaada zikifikia dola bilioni 4.578, huku kiasi cha sasa kinachoendelea kufanya kazi kikiwa ni dola bilioni 2.52 ambazo zinaendelea kuleta msukumo mpya katika ustahimilivu na maendeleo endelevu ya taifa.

No comments