WALLACE KARIA KUMSHAWISHI SAMATTA KUFUTA KAULI YA KUSTAAFU

 


Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, amepanga kukutana na nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta, ili kumshawishi afute kauli yake ya kustaafu kuichezea timu hiyo kwa kuwa taifa bado lina uhitaji mkubwa wa mchango wake. 

Karia alibainisha kuwa alishtushwa na taarifa hizo alizoziona kwenye mitandao ya kijamii na kufafanua kuwa Samatta hajamtaarifu rasmi, jambo linalomfanya amwite mezani kwa ajili ya mazungumzo ya kina akiamini kuwa mchezaji huyo anaweza kubadili uamuzi wake huo. 

Hatua hii inakuja baada ya fowadi huyo mwenye umri wa miaka 33 kutangaza rasmi kuweka kando vifaa vya timu ya taifa akiamini kuwa wakati umefika kwa vipaji vipya kupewa nafasi ya kuisukuma mbele Taifa Stars, huku akiwashukuru Watanzania kwa sapoti kubwa waliyompa katika kipindi chote cha utumishi wake.

Uamuzi huo wa Samatta unahitimisha safari ndefu ya mafanikio makubwa iliyoanzia klabu za African Lyon na Simba, kabla ya kutimkia TP Mazembe ya DRC alikotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wanaocheza ndani mwaka 2015. 

Nyota huyo ambaye kwa sasa anakipiga kunako klabu ya Le Havre nchini Ufaransa, pia aliwahi kung'ara na KRC Genk ya Ubelgiji aliyotwaa nayo ubingwa wa ligi na kiatu cha ufungaji bora mwaka 2019, na baadaye kuweka rekodi ya kihistoria ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England akiwa na Aston Villa, wasifu unaomfanya Karia aamini kuwa uzoefu wake bado ni lulu kwa timu ya taifa.

No comments