Watanzania,Wachina wakumbuka 65 waliofariki wakijenga Tazara



 Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeingia makubaliano rasmi na Jamhuri ya Watu wa China kwa ajili ya kuijenga upya na kuiboresha Reli ya TAZARA. 

Hatua hiyo inalenga kuipa uhai mpya miundombinu hiyo ya kihistoria iliyojengwa kati ya mwaka 1970 na 1975 kama kiungo muhimu cha kiuchumi kanda ya Kusini mwa Afrika.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Patrobas Katambi, wakati wa hafla ya kuwakumbuka wataalamu 65 wa Kichina waliojitolea maisha yao wakati wa ujenzi wa reli hiyo miongo kadhaa iliyopita. 

Akizungumza katika eneo la makaburi ya mashujaa hao yaliyopo Gongolamboto jijini Dar es Salaam, Waziri Katambi alisisitiza kuwa ushirikiano huu ni matunda ya mbegu iliyopandwa na waasisi wa mataifa haya.

Waziri Katambi alieleza kuwa Tanzania, Zambia, na China kwa sasa zinafurahia uhusiano imara wa kijamii na kiuchumi ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Kenneth Kaunda wa Zambia, na aliyekuwa Rais wa China, Mao Ze Dong. 






Aliongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendeleza kwa vitendo msingi huo katika nyanja za teknolojia, uchumi, na siasa, jambo linaloshuhudiwa kupitia miradi mikubwa inayotekelezwa nchini kwa usimamizi wa wataalamu wa Kichina.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,James Millya, ameishukuru Serikali ya China kwa kudumisha urafiki wa dhati na Tanzania. 

Alibainisha kuwa Tanzania inathamini mchango wa China kwa kuwa walijitolea kusaidia kipindi ambacho nchi yao bado haikuwa na uchumi mkubwa, wakitumia rasilimali fedha na nguvu kazi ambapo baadhi ya wataalamu wao walipoteza maisha kwa ajili ya ujenzi wa TAZARA.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, amethibitisha kuwa serikali yake itaendelea kuuenzi na kuuendeleza uhusiano huo wa kihistoria kati ya mataifa hayo matatu. 

Alihitimisha kwa kusema kuwa ushiriki wa China katika miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ni kielelezo cha dhamira yao ya kuona Tanzania ikisonga mbele kiviwanda na kiuchumi.

No comments