Tanzanite Princess Mabingwa Soka la Wanawake Dar



Timu ya Tanzanite Princess imetawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi ya Soka la Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 10-0 dhidi ya Wisdom Queens. 

Katika mchezo huo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki wilayani Ubungo, mabingwa hao walionyesha kiwango cha juu na kumaliza ligi hiyo wakiwa na jumla ya pointi 12. 

Nafasi ya pili imeshikiliwa na Mbagala Queens waliomaliza na pointi 10, huku Rangi Tatu Queens wakifunga mnyororo wa tatu bora kwa kuvuna pointi sita.

Mbali na ubingwa huo, timu ya Tanzanite Princess imeng’ara pia katika tuzo za mmoja mmoja ambapo Fatuma Muhibu ameibuka mfungaji bora wa ligi hiyo huku Leila Juma akitangazwa kuwa kipa bora. 

Washindi hao walikabidhiwa medali za dhahabu pamoja na tuzo zao katika hafla fupi iliyofanyika uwanjani hapo mara baada ya mchezo kukamilika. 

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam, Somoe Ng’itu, alizipongeza timu zote 13 zilizoshiriki akibainisha kuwa ushindani ulioonyeshwa ni kielelezo tosha cha ukuaji wa soka la wanawake mkoani humo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya, aliipongeza Tanzanite Princess na kuwataka kuanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya hatua inayofuata. Nyambaya, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), alisisitiza kuwa mabingwa hao sasa wanakwenda kukutana na ushindani mkali kutoka kwa mabingwa wa mikoa mingine, hivyo wanapaswa kujipanga vyema ili kuendeleza taswira nzuri ya soka la Dar es Salaam kitaifa.

Ligi hiyo iliyoanza kwa hatua ya makundi ilishirikisha timu mbalimbali zikiwemo Kinondoni Queens, The Eleven Stars, Rangi Tatu Queens, Mbagala United, Mtoni Queens, Kigambani Soccer, Mshikamano Queens, Tanzanite Princess, Ilala Queens, Wisdom Queens, Muungano Queens, Evergreen Queens na Mbaga Queens.

 Ushiriki wa timu hizo umetafsiriwa kama hatua muhimu katika kuibua vipaji vipya vitakavyosaidia kuimarisha klabu za ligi kuu na timu za taifa za wanawake siku za usoni.

No comments