Barker, Ibrahim Imoro Wang’ara Tuzo za Machi



Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu ya NBC baada ya kuiongoza timu yake kupata matokeo ya kuridhisha katika mzunguko wa ligi hiyo. 

Katika kinyang’anyiro hicho, Barker amewashinda Pedro Goncalves wa Yanga pamoja na David Ouma aliyekuwa akiinoa Singida Black Stars. 

Mafanikio hayo yametokana na Barker kuiwezesha Simba kushinda michezo miwili na kutoka sare michezo mingine miwili, matokeo yaliyoivusha timu hiyo kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Kwa upande wa wachezaji, beki wa Singida Black Stars, Ibrahim Imoro, ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Machi kutokana na kiwango kikubwa alichokionyesha katika michezo mitano aliyocheza. 

Imoro alifanikiwa kufunga mabao matatu na kuisaidia timu yake kupanda daraja kwenye msimamo wa ligi kutoka nafasi ya 10 hadi ya sita. Katika kura za mchuano huo, beki huyo amewapiku mshambuliaji Anicet Oura wa Simba na Lamine Jarjou wa Singida Black Stars katika tuzo hizo zinazoratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mbali na klabu na wachezaji, kamati ya tuzo imemchagua Meneja wa Uwanja wa Airtel mkoani Singida, Omar Malule, kuwa Meneja Bora wa mwezi huo. 

Malule ametambuliwa kutokana na umakini wake na ufanisi katika usimamizi wa matukio ya michezo pamoja na utunzaji wa miundombinu ya uwanja huo, jambo lililoongeza ubora wa mechi zilizochezwa katika dimba hilo. Tuzo hii inalenga kuhamasisha wasimamizi wa viwanja nchini kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa ajili ya maendeleo ya soka.

Aidha, tuzo hizo zimehusisha pia Ligi ya Championship ambapo mchezaji Omari Mponda wa Mbuni FC ameibuka kidedea kama Mchezaji Bora wa mwezi Machi. 

Mponda alifanikiwa kufunga mabao mawili muhimu ndani ya dakika 155 alizocheza katika michezo miwili, kiwango kilichomfanya awashinde Yusuf Mhilu na Maulid Shaaban wa Geita Gold FC. Mafanikio ya wachezaji hawa na makocha wao yanatajwa kuwa chachu ya kuongeza ushindani katika ligi za hapa nchini kuelekea mwishoni mwa msimu.

No comments