MREMA: TUNA IMANI KUBWA NA TUME YA JAJI CHANDE




Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), John Mrema, ameeleza kuwa na matumaini makubwa na Tume iliyoundwa na Rais chini ya Jaji mkuu mstaafu, Othman Chande, akibainisha kuwa imeundwa na wataalamu wenye weledi na heshima ya hali ya juu.

Akizungumza hivi karibuni, Mrema alisema kuwa hatua ya Rais kuunda tume hiyo ina lengo la kuwasaidia Watanzania na ana imani kuwa itafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ili kutoa matokeo yatakayolinufaisha taifa kwa ujumla.

Alibainisha kuwa weledi wa wajumbe wa tume hiyo si wa kutiliwa shaka, akitolea mfano utendaji wa Jaji Chande katika Tume ya Haki Jinai ya mwaka 2023. Alisema mapendekezo ya tume hiyo yalikuwa na tija na yalibadili kwa kiasi kikubwa mwenendo wa mfumo wa haki jinai nchini.

“Hawa ni watu wanaominika ndani na nje ya nchi kwani hawana madoadoa. Hii inanifanya niamini kwamba tume hii itafanya kazi yake kwa umakini mkubwa,” alisema Mrema na kuongeza kuwa uwepo wa watu kama Profesa Juma, Luteni Jenerali mstaafu Meela, na Balozi Ombeni Sefue ni kielelezo cha uzito wa tume hiyo.

Mrema alisisitiza kuwa wajumbe hao ni watu waliojenga sifa na heshima kubwa kitaifa na kimataifa, hivyo hawatakuwa tayari kuharibu rekodi zao. Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa wananchi na wadau wengine kuipa tume hiyo nafasi ya kutimiza wajibu wake.

“Ni muhimu sana kwa wananchi wa nchi hii kuipa nafasi tume itimize wajibu wake ije na ripoti, ili kama taifa sasa tukishajua tulijikwaa wapi, tuanze kutafuta majawabu. Lengo ni kusogea mbele tukiwa wamoja kama nchi moja ambayo haina ubaguzi wa 'mjomba wala shangazi',” alisisitiza.

Alimalizia kwa kusema kuwa Tume ya Jaji Chande imebeba maslahi mapana ya nchi na inaundwa na wazalendo wa kweli ambao historia ya nchi itakuja kuwakumbuka kwa mchango wao katika mustakabali wa taifa.

No comments