WAKILI KIPANGULA: AMANI KUHATARISHWA NA UANDISHI UNAPUUZA MAADILI



KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Patrick Kipangula, ametahadharisha kuwa uandishi wa habari unaopuuza maadili ya taaluma unaweza kuhatarisha umoja wa kitaifa, amani na utulivu wa kijamii.

Kipangula alisema hayo katika kikao cha viongozi na wanachama wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN), Jumuiya ya wanahabari wa mitandao ya kijamii Tanzania (JUMIKITA)  na Mtandao wa Redio za  Kijamii Tanzania (TADIO) kilichofanyika Dar es salaam Aprili 17.

Akizungumza  Kipangula alisema waandishi wa habari hawana budi kutambua uzito wa wajibu wao hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Alibainisha kuwa habari zinazosambazwa na vyombo vya habari zina mchango mkubwa katika kuibua maoni kwa umma na kuathiri umoja nwa kitaifa.

Alieleza kuwa amani inaakisi kutokuwepo kwa migogoro na vurugu, wakati utulivu unamaanisha wananchi wanaweza kuishi kwa usalama na uhakika bila woga. 

Alisema vitu hivyo vinategemea umoja wa kitaifa unaojengwa katika mshikamano miongoni mwa watu bila kujali tofauti zao za kiitikadi na kidini.



Kipangula alionya kuwa taarifa zisizo na maadili zinaweza kuchochea mgawanyiko, kupotosha umma na kudhoofisha umoja wa kijamii. 

Aliwataka waandishi wa habari kuzingatia weledi, uadilifu na uwajibikaji katika kazi zao ili kuepuka kuharibu umoja wa nchi.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina jukumu la msingi la kukusanya, kuchakata na kupeana taarifa sahihi, huku vikisaidia kuibua mitazamo ya umma kwa njia zinazohimiza maelewano na maendeleo.

Pia alisisitiza haja ya kuzingatia kwa dhati kanuni ya maadili ya uandishi wa habari, ambayo inakuza ukweli, haki, uwazi na kuheshimu haki za binadamu, maadili ambayo alisema ni muhimu kwa kulinda amani, kuimarisha utulivu na kudumisha umoja wa kitaifa.

No comments