Mikakati ya Serikali kumarisha mazingira ya biashara kwa Mwaka wa Fedha 2026/27



Katika mwaka ujao wa fedha, serikali imepanga kutekeleza mkakati kabambe wa kuimarisha mazingira ya biashara nchini kwa kuleta Sheria mpya ya Uwekezaji wa Umma itakayotoa muundo imara wa usimamizi wa rasilimali na mitaji ya taifa.

Mkakati huu unajumuisha uanzishwaji wa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma utakaosaidia kuongeza thamani ya mashirika ya serikali na kuhakikisha yanajiendesha kwa faida na kutoa gawio stahiki.

Vilevile, serikali inatarajia kukamilisha uandaaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) ambao utakuwa daraja la kwanza kuelekea utekelezaji wa Dira ya 2050, ukizingatia zaidi sekta za kipaumbele kama viwanda, teknolojia ya habari, na nishati safi ili kuchochea mapinduzi ya viwanda nchini.

Hayo yamesemwa na  Profesa Kitila Mkumbo wakati akisoma Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Bungeni leo.

Mkakati mwingine wa kipaumbele ni matumizi ya teknolojia ya hali ya juu kupitia Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mipango ya Maendeleo (NPMIS) ambao utatumika kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kielelezo na kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa bila ubadhirifu.

Serikali pia imepanga kuimarisha vituo vya huduma ya mahala pamoja (One Stop Service Centers) ili kurahisisha mchakato wa usajili wa wawekezaji na kupunguza vikwazo vya kiritimba ambavyo vimekuwa vikichelewesha kuanza kwa miradi mikubwa.

Kupitia Tume ya Taifa ya Mipango, kutakuwepo na mkakati wa makusudi wa kukuza uwekezaji kwenye maeneo ya mipakani na miji inayokua kwa kasi ili kusambaza fursa za kiuchumi nchi nzima na kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na ukuaji wa uchumi wa taifa lake.

Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imeliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 174.59 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2026/27. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 94.67 zimepangiwa matumizi ya kawaida yakijumuisha mishahara na uendeshaji wa ofisi, huku shilingi bilioni 79.91 zikielekezwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo.

No comments