MBINU CHAFU ZA WANASIASA,MITANDAO ZATAJWA GHASIA ZA OKTOBA 29
Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025, imeweka hadharani mkakati wa kundi la wanasiasa na wanaharakati uliotumika kuchochea ghasia nchini. Ripoti hiyo imebaini kuwepo kwa vichocheo vinane vilivyotumika kwa makusudi kupandikiza hasira miongoni mwa wananchi.
Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Magogoni leo Aprili 23, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, alisema baadhi ya wanasiasa walitumia changamoto za maisha zinazowakabili wananchi kama fursa ya kuwashawishi kushiriki ghasia kupitia kauli mbiu na matamko mbalimbali yenye mrengo wa uasi.
Jaji Chande alitaja baadhi ya kauli hizo kuwa ni pamoja na ‘No reform no election’, ‘Samia must go’, na ‘Tunahakikisha nchi haisimami mpaka serikali iondoke’. Alibainisha kuwa kauli hizi zililenga kuaminisha umma kuwa serikali imepoteza uhalali na kwamba hakuna haja ya kufanyika kwa uchaguzi bila mabadiliko ya mfumo.
Aidha, ripoti hiyo imemulika matumizi ya mitandao ya kijamii kama chombo kikuu cha kuratibu ghasia hizo. Jaji Chande alieleza kuwa wabunifu wa mada mtandaoni walihamasisha wananchi kutoshiriki uchaguzi mkuu na kupanga mbinu za kuhujumu mchakato mzima.
Aliongeza kuwa baadhi ya washiriki wa ghasia walikiri kupewa simu maalumu za mkononi kwa ajili ya kupiga picha za majeruhi, vifo, na harakati za magari ya jeshi ili kutoa taswira potofu mtandaoni na kuibua hasira zaidi kwa wananchi.
Mwenyekiti huyo pia alibainisha kichocheo kingine kuwa ni wanasiasa waliokatwa majina yao katika mchakato wa kuwania ubunge na udiwani ndani ya vyama vyao. Watu hao walitajwa kuhamasisha ghasia hizo chinichini kwa matumaini kuwa vurugu hizo zingesaidia kuleta mabadiliko ya mfumo utakaowabeba.

Post a Comment