Ilala yapongezwa kujiandaa kupokea wanafunzi 2028



Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda ameipongeza Manispaa ya Ilala kwa kuanza maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2028, kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Kitunda Relini.

Ametoa pongezi hizo leo Aprili 13, 2026 alipofika wilayani Ilala kukagua mradi huo, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha utayari na maono ya muda mrefu ya halmashauri katika kukabiliana na ongezeko la wanafunzi litakalotokana na mfumo wa Double Cohort.

Katika maelezo ya mradi huo, imeelezwa kuwa Ilala imejikita katika kuandaa miundombinu ya kutosha kwa ajili ya wanafunzi watakaohitimu darasa la sita na darasa la saba kwa pamoja mwaka 2027 na kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2028, hali inayotarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi kwa kiasi kikubwa.



Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitunda Relini unahusisha jengo la ghorofa linalotekelezwa na mkandarasi MNICO Construction (T) Ltd, ukiwa na madarasa 16, matundu 53 ya vyoo, ofisi 12 za walimu, stoo mbili, maabara nne za sayansi, chumba cha TEHAMA na maktaba. 

Ujenzi huo unalenga kuongeza nafasi za wanafunzi pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Ujenzi wa shule hiyo ulianza rasmi Novemba 29, 2024 na unatarajiwa kukamilika Mei 31, 2026, ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha miundombinu inakuwa tayari kabla ya mwaka 2028.

Kwa upande wa gharama, mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.21, ambapo fedha hizo zinatokana na Serikali Kuu kupitia mradi wa SEQUIP pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Ilala. 

Hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 3.82 zimepokelewa na zaidi ya shilingi bilioni 3.59 tayari zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za sekondari za Kitunda, Makalamengi, Kipunguni na Minazi Mirefu pamoja na maeneo mengine ya katikati ya jiji. 



Aidha, utaongeza ubora wa elimu kwa kuweka mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Sambamba na hilo, wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya CRDB wanatarajiwa kuchangia madawati kwa ajili ya maandalizi ya kupokea wanafunzi hao, huku klabu za kupinga rushwa zikianzishwa shuleni ili kukuza maadili kwa wanafunzi.

Akihitimisha, Mwang’onda ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kuhakikisha changamoto za miundombinu zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu cha kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji na uzalendo, huku miradi kama huu wa Kitunda Relini ukiwa kielelezo cha maandalizi sahihi ya kukabiliana na changamoto za baadaye.


No comments