AMANI NA MARIDHIANO: ASKOFU MNDOLWA ATUMIA MATHAYO 18:15 KUELEZA TANZANIA HAIJASHINDWA KUJITIBU




Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mh. Mahimbo Mndolwa, ametoa wito wa kulinda amani, utulivu na mshikamano wa taifa, huku akipongeza hatua ya ukomavu iliyofikiwa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kushughulikia changamoto za ndani kwa kutumia mifumo ya kitaifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Aprili 13, 2026, Askofu Mndolwa ameziba mianya ya watu wanaotaka Tanzania iingiliwe na mataifa ya nje, akisisitiza kuwa taifa bado halijashindwa kujiongoza. Amepongeza kuundwa kwa Tume huru ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akitaja hatua hiyo kama alama ya ujasiri na busara ya uongozi.

Msingi wa Maandiko: Mathayo 18:15

Katika kutilia mkazo umuhimu wa utatuzi wa migogoro kuanzia ngazi ya ndani, Askofu Mndolwa amenukuu maandiko matakatifu kutoka Mathayo 18:15, yanayosisitiza utaratibu wa kufuata pale ndugu anapokukosea.

"Hata katika familia, lazima muanze nyinyi wenyewe. Mathayo 18:15 inasema ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonye wewe na yeye peke yenu. Mkianza wenyewe, mnaonyesha ukomavu mkubwa... Tanzania ni taifa huru tangu zamani, na kuanza kwetu wenyewe kutatua changamoto zetu ni ishara kuwa tunaelekea mahali sahihi," alisisitiza Askofu Mndolwa.

Ujumbe kwa Mataifa ya Nje na Umoja wa Kimataifa

Akielezea uzoefu wake katika majukwaa ya kimataifa kama mwakilishi wa Anglikana katika Umoja wa Mataifa (UN), Askofu Mndolwa ameweka wazi kuwa Tanzania imeendelea kuonyesha uwezo wa kujitathmini. Alibainisha kuwa walipoulizwa kwanini hawakaribishi mataifa mengine kuingilia kati, jibu limekuwa wazi: "Tutawaita pale tutakaposhindwa, lakini kwa sasa hatujashindwa... hata kanisani tunaanza wenyewe."

Pongezi kwa Rais Samia na Tume

Askofu Mkuu amempongeza Rais Samia kwa uteuzi wa wajumbe wa Tume hiyo, akisema kuwa aina ya watu waliochaguliwa inatoa matumaini ya kufikia hitimisho la haki kwa maslahi ya taifa. Amesema kuwa uamuzi huo si tu wa kisheria, bali ni wa kiroho na kizalendo unaolenga kuimarisha maridhiano na mshikamano wa kitaifa ambao ndio nguzo kuu ya utulivu wa Tanzania kwa sasa.

Kiongozi huyo amemshukuru Mungu kwa hatua hii kubwa, akisema kuwa ni ukomavu kwa taifa kushughulikia changamoto zake bila kushinikizwa, jambo ambalo linaendelea kuifanya Tanzania kuwa kioo cha amani barani Afrika.

No comments