Dkt. Chakwera Akutana na Viongozi wa Vyama vya Siasa Zanzibar, Avutiwa na Utamaduni wa Vijana
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera, leo Aprili 13, 2026, amewasili visiwani Zanzibar na kufanya mfululizo wa mazungumzo na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.
Ziara hiyo ambayo ni sehemu ya mikakati ya Jumuiya ya Madola kuimarisha demokrasia na mashirikiano nchini Tanzania, imemkutanisha Dkt. Chakwera na viongozi wenye ushawishi mkubwa katika ulingo wa siasa za Zanzibar ili kubadilishana mawazo juu ya mustakabali wa amani na maendeleo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mchana wa leo, Dkt. Chakwera amekutana na viongozi waandamizi akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa na Mwenyekiti wa ADA-TADEA, Juma Khatibu, pamoja na mwanzilishi wa chama cha ADC, Hamad Rashid.
Aidha, viongozi wengine walioshiriki ni Mwenyekiti wa chama cha AAFP, Said Soud Said, na Katibu Mkuu wa Chama cha Makini, Ameir Ameir, ambapo kwa pamoja wamejadili umuhimu wa kuimarisha misingi ya maridhiano na umoja wa kitaifa katika kuendesha shughuli za kisiasa visiwani humo.
Mbali na masuala ya kidiplomasia na kisiasa, Mhe. Dkt. Chakwera alipata fursa ya kipekee ya kujionea maisha ya kila siku na utamaduni wa vijana wa Zanzibar alipotembelea eneo maarufu la mchezo wa Makachu.
Akiwa hapo, ameshuhudia vijana wakionesha ufundi wao wa kuchupa (dive) katika Bahari ya Hindi, mchezo ambao si burudani tu, bali umekuwa ukitumika na vijana hao kama jukwaa la kutoa ujumbe maalum wa kijamii na kiutamaduni, jambo lililomvutia mjumbe huyo wa Jumuiya ya Madola.
Ziara hii ya Dkt. Chakwera inaendelea kuimarisha taswira ya Tanzania kama mdau muhimu wa Jumuiya ya Madola, huku ikionyesha utayari wa viongozi wa Zanzibar katika kushirikiana na taasisi za kimataifa.
Baada ya kukamilisha ratiba yake visiwani humo, mjumbe huyo anatarajiwa kuendelea na mikutano mingine na wadau wa maendeleo, akisisitiza ujumbe wa amani na mshikamano ambao ndio nguzo kuu ya Jumuiya ya Madola kote duniani.


Post a Comment