BFT YARIDHIKA NA UFUNDI MASHINDANO YA TAIFA YA NGUMI 2026
Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) limetangaza kukamilika kwa mafanikio makubwa kwa Mashindano ya Wazi ya Ubingwa wa Taifa 2026, yaliyofikia tamati juzi katika viwanja vya Chuo cha Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, ameeleza kuwa uongozi umeridhishwa na kiwango cha juu cha nidhamu na ufundi wa kisasa ulioonyeshwa na mabondia wa kiume na kike, hatua inayothibitisha maendeleo ya mchezo huo katika kuibua vipaji vipya vitakavyoiwakilisha Tanzania kwenye medani za kimataifa.
Katika mfululizo wa fainali za kusisimua kwa upande wa wanaume, klabu ya MMJKT imeibuka kidedea kwa kunyakua ushindi katika madaraja mengi, ikianzia na Juma Athumani aliyemshinda Salum Awadh kwa pointi 5-0 (kilo 48). Mafanikio hayo yaliendelezwa na Mohamedi Juma aliyemshinda Rasidi Rashidi katika uzani wa kilo 71, huku Elankunda Daniel akimchapa Enzi Kaseleleka wa Magereza kwa pointi 3-2 (kilo 80). Aidha, klabu hiyo ilihitimisha kwa kishindo katika uzani wa juu baada ya Abdallah Kassim na Maximilian Oloo kuwashinda wapinzani wao kwa KO katika uzani wa kilo 92.
Klabu ya Ngome nayo imeonyesha upinzani mkali baada ya Japhet Alon kumshinda Muhsin Hassan wa MMJKT kwa uamuzi wa mwamuzi (RSC) ndani ya raundi ya kwanza katika uzani wa kilo 54, huku Yusufu Abdurahmani akimshinda Bakari Omari kwa pointi 3-2 (kilo 57). Julius Mtembezi aliongeza ushindi mwingine kwa Ngome baada ya kumzidi Shamte Mwaram wa MMJKT kwa pointi 3-2 katika uzani wa kilo 67, jambo lililozifanya klabu hizi mbili za majeshi kuwa mhimili wa mashindano ya mwaka huu kutokana na ubora wa mabondia wao.
Matokeo mengine muhimu yalimhusisha Omari Saidi wa Daba aliyemshinda Abdallah Hasani kwa pointi 5-0 (kilo 51), na Asubuhi Jumanne wa Magereza aliyemchakaza Paulo Sangu kwa pointi kama hizo (kilo 60). Kwa upande wa wanawake, ushindani ulitawaliwa na Zulfa Macho wa Ngome aliyemshinda Enifa Jackson wa MMJKT kwa pointi 5-0 (kilo 52), huku Aisha Iddi wa MMJKT akijinyakulia ushindi katika uzani wa kilo 50. Mashindano haya yanatajwa kuwa chachu ya kuimarisha timu ya taifa ya ngumi kuelekea mashindano mbalimbali ya kikanda na kimataifa yajayo.

Post a Comment