MPOGOLO: MWENGE WA UHURU NI CHACHU YA MAENDELEO NA AMANI
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali katika kudumisha amani, umoja na mshikamano huku zikichochea kasi ya maendeleo kupitia miradi ya kimkakati.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa mchakamchaka, Mpogolo amebainisha kuwa Mwenge huo unakimbizwa kwa umbali wa kilometa 54 ukiwa na lengo la kuhakikisha ukifika katika nyanja zote za huduma za kijamii zinawafikia wananchi kwa ufanisi na weledi mkubwa.
Mapokezi ya Mwenge huo yalianza kwa shamrashamra kubwa alfajiri ya leo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Terminal 1, ambapo baada ya mapokezi hayo viongozi na wananchi wakanza mchakmchaka wa ukaguzi na uzinduzi wa miradi saba yenye thamani ya Shilingi bilioni 51.825.
Mpaka sasa, Mwenge huo umeshapita katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kariakoo kwa ajili ya uzinduzi wa mradi wa kitega uchumi utakaoinua biashara ndogondogo, pamoja na kukagua ujenzi wa barabara ya Lindi kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.015.
Katika kuimarisha huduma za afya na elimu, mbio hizo mchana huu zinaelekea kuzindua mradi wa kisima cha maji na kituo cha afya Mchikichini, sambamba na ufunguzi wa shule ya sekondari Kitunda Relini na kituo cha polisi Bonyokwa kwa ajili ya ulinzi wa raia.
Mkuu wa Wilaya amewapongeza wananchi na vikundi vya vijana kama Fighters wa Segerea kwa kujitokeza kwa wingi kuonyesha shughuli zao za kimaendeleo, jambo linaloendana na kaulimbiu ya mwaka huu inayosisitiza kuwa Tanzania ni yetu sote na tushikamane kuleta maendeleo.
Ratiba ya mbio hizi za kizalendo inatarajiwa kuhitimishwa usiku wa leo kwa mkesha maalum katika eneo la Tabata, ambapo ujumbe wa Mwenge wa Uhuru kuhusu mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, dawa za kulevya, lishe na rushwa utasomwa kwa umma. Baada ya kukamilisha shughuli zake Ilala, Mwenge huo utakabidhiwa kesho Aprili 14 katika Wilaya ya Kigamboni ukiendelea na ziara yake ya umbali wa kilometa 392.22 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya kuelekea mkoani Pwani Aprili 18.
Post a Comment