Adam Atamani Amani kuendelea kuenziwa na kuwa na Mshikamano wa Kitaifa



Msanii wa filamu nchini, Daniel Lufingo, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii ‘Adam’, ametoa wito wa dhati kuhusu umuhimu wa kulinda amani akiamini kuwa ndiyo msingi mkuu wa ustawi wa jamii na tasnia ya sanaa. 

Lufingo amebainisha kuwa amani ya kweli haitokei tu kwa bahati, bali hujengwa juu ya msingi imara wajibu ambapo kila mwananchi anapaswa kutekeleza . Kwake yeye, amani na wajibu ni vitu visivyotenganika, na pale kila mmoja anapotimiza sehemu yake, taifa linapata utulivu unaohitajika kwa maendeleo.

Katika maelezo yake, msanii huyo ameweka wazi kuwa bila utulivu, sekta mbalimbali ikiwemo sanaa zinajikuta katika wakati mgumu kwa sababu wasanii wanategemea uhusiano mzuri na jamii pamoja na serikali. 

Amesema kuwa jamii ndiyo inayopokea na kuthamini kazi zao, huku serikali ikiwa kama mlezi, hivyo kukosekana kwa amani kunasababisha shughuli za kimaendeleo kusimama na kuwaacha wadau wa sanaa kwenye njia panda. 

Ni kupitia utulivu pekee ndipo sanaa inaweza kuchanua na kutoa mchango wake kwa taifa.

Lufingo pia amegusia safari ya taifa kujijenga upya kufuatia changamoto zilizojitokeza baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza umuhimu wa kuponya majeraha na kurejesha umoja. 

Amehimiza kuwa huu ni wakati wa kila mmoja kuchangia katika ujenzi wa mshikamano wa kitaifa ili kuliweka taifa katika hali ya usalama zaidi. 

Kwa upande wa vijana, amewahamasisha kuwa na ari ya kushiriki katika siasa na maendeleo kwani wao ndio nguvu inayoliongoza taifa kuelekea kesho yenye matumaini.

Lufingo amesisitiza kuwa tofauti za kidini, kikabila au kisiasa hazipaswi kuwa kikwazo cha maendeleo, kwani jamii ya sasa imepiga hatua kubwa kielemu na ina uelewa mpana wa mambo. Ameshauri kuwa mazungumzo jumuishi ndiyo njia bora zaidi ya kutatua changamoto zilizopo. 


No comments