MSIGWA: TUNAJALI NA TUMEJIPANGA USALAMA MAJINI

 



Katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi wa majini unaenda sambamba na usalama wa maisha ya wananchi, Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya uokoaji na mawasiliano katika Maziwa Makuu.

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha kuwa ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uratibu wa Masuala ya Utafutaji na Uokozi (MRCC) katika Ziwa Victoria umefikia asilimia 98, huku vituo vidogo vitatu vya uokoaji (SAR) vikijengwa Kanyara (91%), Ukerewe (85%), na Musoma (91%).

Hatua nyingine ni ununuzi wa boti maalum ya wagonjwa (Ambulance Boat) kwa ajili ya Ziwa Victoria, ambayo tayari imewasili na iko tayari kutoa huduma kama hospitali inayotembea majini.

Gharama za usalama pia zimehusisha ununuzi wa boti nyingine nne za uokoaji zilizosambazwa katika Ziwa Tanganyika, Victoria, na Ukanda wa Bahari ya Hindi (Tanga) ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga.

Pamoja na miundombinu hiyo, serikali inaendelea na ujenzi wa minara mitatu ya mawasiliano katika visiwa vya Soswa (50%), Kunene (50%), na Kweru (70%) ndani ya Ziwa Victoria ili kuimarisha tahadhari za hali ya hewa na uratibu wa dharura.

Kwa ujumla, msemaji huyo wa serikali amesema uwekezaji huo wa zaidi ya shilingi trilioni moja katika sekta nzima unalenga kuhakikisha usafiri wa majini unakuwa salama na wa kisasa.

Hii inatoa uhakika kwa wasafiri na wafanyabiashara, jambo linalochochea watu wengi zaidi kutumia usafiri wa majini bila hofu ya usalama wa maisha yao.

No comments