DAR CITY YAWEKA KAMBI KWA AJILI YA BAL



 Maandalizi ya mabingwa wa mpira wa kikapu nchini, Dar City, kwa ajili ya mashindano ya Ligi ya Kikapu Afrika (BAL), yamepamba moto huku timu hiyo ikiweka kambi ya nguvu visiwani Zanzibar. 

Kocha Msaidizi wa kikosi hicho, Mohamed Mbwana, amethibitisha kuwa hali ya kambi ni shwari na wachezaji wana ari kubwa ya kuonesha ushindani wa hali ya juu katika anga za kimataifa.

Kikosi hicho, ambacho kinatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea Pretoria, Afrika Kusini, kimekuwa kikijifua visiwani humo ili kuboresha ujuzi na mbinu za mchezo. Mashindano hayo ya msimu wa sita wa BAL yanatarajiwa kuanza kurindima Machi 27 hadi Aprili 5, mwaka huu, huku Dar City ikibeba dhamana ya kuwakilisha bendera ya Tanzania.

Akizungumza kwa njia ya simu akiwa kambini, Mbwana amesema kuwa tangu kuanza kwa mazoezi mwezi Januari jijini Dar es Salaam, uwiano wa timu umeimarika kwa kiasi kikubwa. Aliongeza kuwa uamuzi wa kuhamishia kambi Zanzibar ulikuwa ni mkakati wa benchi la ufundi kubadilisha mazingira na kutumia vifaa bora vya ndani, jambo ambalo limeongeza ari na ubora wa mazoezi kwa wachezaji.

Benchi la ufundi la Dar City linaongozwa na Kocha Mkuu, Momodou Gueye, akisaidiwa na Nabil Kabalan, kocha mwenye uzoefu aliyewahi kukipiga katika klabu ya Al Ahly Benghazi. Uzoefu wa makocha hao unatajwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiufundi yaliyoonekana ndani ya kikosi hicho katika kipindi kifupi cha maandalizi.

Mbwana amehitimisha kwa kusema kuwa Dar City haitaenda Afrika Kusini kushiriki tu, bali kupambana na kuiletea nchi heshima. Amebainisha kuwa juhudi za wachezaji na miongozo ya walimu wao ndiyo itakayokuwa silaha kubwa ya kupata matokeo chanya dhidi ya timu nyingine kubwa za Afrika zitakazokusanyika Pretoria wiki ijayo.

No comments