KAZI NA UTU: RAIS SAMIA AMFIKIA NGULI HASSAN BITCHUKA NYUMBANI KWAKE
Katika kuonesha kuwa mchango wa magwiji wa sanaa nchini hausahauliki, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemjulia hali na kumpatia mkono wa pole mwanamuziki nguli wa mionzi ya dansi, Hassan Bitchuka.
Salamu hizo za faraja pamoja na msaada wa Shilingi milioni 10 zimefikishwa nyumbani kwa nguli huyo eneo la Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (Mwana FA), aliyemwakilisha Rais.
Sauti ya Dhahabu, Tuzo ya Heshima
Bitchuka, ambaye sauti yake imepamba bendi kongwe kama DDC Mlimani Park Orchestra (Sikinde), Msondo Ngoma, na OSS, amekuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda sasa. Akikabidhi msaada huo wa fedha kwa ajili ya matibabu, Naibu Waziri Mwinjuma alibainisha kuwa Rais anathamini mchango usiopimika wa msanii huyo katika kuelimisha taifa kwa miongo mingi.
"Rais Samia amenituma nifike hapa kukuletea salamu zake za pole na upendo. Anakuombea upate nafuu ya haraka na ameelekeza nikukabidhi kiasi hiki kwa ajili ya kusaidia taratibu zako za matibabu na kukutia moyo," alisema Mwinjuma wakati wa makabidhiano hayo.
Shukrani za Gwiji
Kwa upande wake, Bitchuka alipokea msaada huo kwa mguso wa kipekee, akimshukuru Rais Samia kwa moyo wake wa kuwakumbuka wasanii wakongwe. Tukio hili linatafsiriwa na wadau wa sanaa kama kurejesha heshima ya taaluma ya muziki nchini, likiendeleza falsafa ya "Kazi na Utu" kwa vitendo.
Muendelezo wa Kugusa Maisha ya Wasanii
Hatua hii kwa Hassan Bitchuka imekuja ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Rais Samia kuwajali wadau wa sanaa na familia zao. Katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Rais alimzawadia mama mzazi wa marehemu Steven Kanumba, Bibi Flora Mtegoa, gari jipya aina ya Harrier (New Model).
Zawadi hiyo kwa mama Kanumba ni ishara ya kuthamini alama kubwa aliyoiacha marehemu mwanawe katika tasnia ya filamu nchini, jambo linaloonesha kuwa serikali imejipanga kuimarisha mifumo ya ustawi kwa wasanii waliolitumikia taifa kwa uaminifu.
Post a Comment