Kompyuta imechemka, Senegal yaituliza Morocco na kutwaa ubingwa wa AFCON
Senegal wametawazwa kuwa wafalme wa soka barani Afrika kwa mara ya pili katika historia yao baada ya kuichapa wenyeji Morocco bao 1–0. Ushindi huo uliopatikana baada ya dakika 120 za kusisimua katika fainali ya TotalEnergies Africa Cup of Nations (AFCON) iliyopigwa jijini Rabat.
Anguko la Utabiri wa Kompyuta
Licha ya teknolojia na kompyuta za kisasa za kutabiri matokeo (Supercomputers) kuipa Morocco nafasi ya juu ya asilimia 19% kutwaa ubingwa huo kutokana na faida ya kucheza nyumbani, Senegal wamethibitisha kuwa soka huchezwa uwanjani na si kwenye kanuni za kimahesabu.
Utabiri huo ambao uliowaona "Simba wa Atlas" kama timu tishio zaidi barani, uliangushwa na nidhamu ya hali ya juu ya vijana wa Pape Thiaw ambao walionyesha kuwa uzoefu na moyo wa kupambana ni silaha tosha dhidi ya yeyote.
Ushindi huu wa Senegal umekuwa fundisho kwa wachambuzi wa takwimu, kwani dakika 120 za Rabat zimefuta kabisa asilimia na namba zilizokuwa zikiipendelea Morocco kabla ya kipyenga cha kwanza.
Wakati mitambo ikitazama rekodi ya Morocco ya kutofungwa nyumbani kwa miongo kadhaa, Senegal walitazama nyota yao ya pili, wakipindua meza na kuacha mitambo hiyo ikiwa haina jibu mbele ya shuti kali la Pape Gueye lililoandika historia mpya.,
Dakika za Hatari na Shujaa Pape Gueye
Wakati mchezo ukiingia kwenye muda wa nyongeza baada ya suluhu ya 0-0, shujaa wa mchezo Pape Gueye alihitaji dakika tatu pekee za kipindi cha kwanza cha muda wa ziada kuamua hatma ya mchezo. Gueye aliachia shuti kali la mguu wa kushoto kutokea nje ya 18 lililomshinda mlinda mlango Yassine Bounou, na kuzizima kelele za maelfu ya mashabiki wa Morocco waliofurika uwanjani hapo.
Penalti Iliyokosa na Ukuta wa Mendy
Morocco walikuwa na nafasi ya dhahabu kumaliza mchezo ndani ya dakika 90 za kawaida. Baada ya marejeo ya VAR, wenyeji walizadiwa penalti dakika za lala salama. Hata hivyo, kipa Edouard Mendy alionyesha umahiri wake kwa kupangua mkwaju wa Brahim Diaz, na kuwalazimu Morocco kwenda muda wa ziada ambao haukuwa na bahati kwao.
Mtiririko wa Mchezo
Kipindi cha Kwanza: Senegal walianza kwa kasi, wakimfanya kipa Yassine Bounou kufanya kazi ya ziada kuokoa kwanza kichwa cha Gueye na kisha shuti la ana kwa ana la Iliman Ndiaye.
Kipindi cha Pili: "Simba wa Atlas" (Morocco) walirejea kwa kasi, huku Ayoub El Kaabi akikosa nafasi ya wazi baada ya pasi maridadi kutoka kwa Bilal El Khannouss.
Dakika za Mwisho: Kipa Bounou aliendelea kuwa kikwazo kwa Senegal baada ya kuokoa shuti la Ibrahim Mbaye katika dakika ya 89.
Safari ya Bao la Ushindi
Bao la ushindi lilitokana na makosa ya kiungo wa Morocco, ambapo Sadio Mané aligusa mpira kwa kisigino kumpata Idrissa Gana Gueye, aliyemlisha Pape Gueye. Kiungo huyo alionyesha nguvu na utulivu kabla ya kupiga shuti lililozama wavuni.
Licha ya juhudi za En-Nesyri na Diaz kutaka kusawazisha, ukuta wa Senegal uliokuwa na nidhamu ya hali ya juu ulisimama imara hadi kipyenga cha mwisho.
Kauli ya Mchezaji Bora wa Mechi – Pape Gueye
"Nina furaha sana kushinda fainali hii; ulikuwa mchezo mgumu sana. Baada ya Morocco kukosa penalti, tulibaki na umakini na kucheza soka letu la Kisenegal. Kufunga katika fainali ni jambo la fahari kwangu, na la muhimu zaidi ni kwamba timu ya taifa ya Senegal sasa ina nyota ya pili kifuani."

Post a Comment