HUZUNI ZATAWALA MUIGIZAJI NA MTAYARISHAJI MAHIRI WA SINEMA ALLWELL ADEMOLA AKIPUMZISHWA NYUMBA YA MILELE




Muigizaji na mtayarishaji mahiri wa sinema nchini Nigeria , Allwell Ademola, Januari 9,2026 amepumzishwa katika nyumba yake ya milele  katika makaburi ya Atan yaliyopo Yaba, Lagos, nchini Nigeria.

maziko yake yalihudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo mastaa wakubwa wa tasnia hiyo akiwamo Toyin Abraham, Biola Adebayo, Rotimi Salami, Saidi Balogun, na wasanii wengine wengi.

Kabla ya maziko hayo ya Ijumaa, mastaa wa Nollywood na mashabiki walikusanyika Alhamisi kwa ajili ya ibada ya nyimbo, maandamano ya mishumaa pamoja na maombi maalum (wrap prayer) kwa ajili ya kumkumbuka mpendwa wao. Familia na waombolezaji wengi walivaa mavazi meupe ikiwa ni ishara ya kumuenzi msanii huyo aliyekuwa na ushawishi mkubwa.

Ademola anaripotiwa kufariki dunia Desemba 27, 2025, kwa ugonjwa wa moyo akiwa nyumbani kwake Lagos muda mfupi baada ya kulalamika kuwa anashindwa kupumua. Kifo chake kimekuwa pigo kubwa kwani alifariki akiwa na umri wa miaka 49, muda mfupi baada ya kuposti video kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram akisema, "mwaka huu hautaona mwisho wangu."

Safari yake ya Sanaa na Maisha 

Allwell Ademola alizaliwa Agosti 9, 1976, jijini Lagos na anatoka katika familia mashuhuri ya Kiyoruba, akiwa mjukuu wa Adetokunbo Ademola, aliyekuwa Jaji Mkuu wa kwanza wa Nigeria. Safari yake ya sanaa ilianza tangu utotoni mwaka 1985 alipoonekana kwenye vipindi vya televisheni vya watoto kama "Tales by Moonlight."

Alianza rasmi kuigiza kwenye filamu za Nollywood mwaka 1992 na alijipatia sifa nyingi kupitia filamu kama You or I (2013), Omo Emi (2017), na Ile Wa (2018). Allwell alikuwa msanii wa kipekee aliyeweza kuigiza kwa lugha ya Kiingereza na Kiyoruba, huku akijihusisha pia na uandishi wa miswada na uongozaji wa filamu kupitia kampuni yake ya "Allwell Ademola Production."

Mbali na uigizaji, Allwell alikuwa na kipaji cha muziki ambapo mwaka 2002 aliunda bendi yake iitwayo "Allwell and Company" na kutoa albamu mwaka 2006.







Simanzi ya Familia na Marafiki 

Kaka wa marehemu, Adeboyega Adebayo, ameeleza kuwa bado hajakubali kwamba dada yake amefariki dunia kwani hakuwa dada tu bali alikuwa rafiki wa karibu. Amemuelezea Allwell kama mtu aliyekuwa na ujasiri mkubwa, asiyekubali kuonewa, na aliyekuwa na ari ya kufika mbali katika sanaa.

"Alikuwa shujaa, mwenye nguvu na aliyependa sana kile alichokuwa akikifanya. Hata bila kwenda shule ya kuzungumza, alikuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza mbele ya umati wa watu," alisema Adeboyega.

Tasnia ya filamu nchini Nigeria na mashabiki wa Nollywood kote barani Afrika wataendelea kumkumbuka Allwell Ademola kwa mchango wake mkubwa kwenye sanaa, ucheshi wake, na uwezo wake wa kipekee wa kuibua vipaji vipya nchini humo.

Baadhi ya Sinema alizoshiriki

Láròdá òjò (2008) kama Agbanimoran

Eti Keta (2011) kama Mama Adigun (pia aliandika)

Lagos Girls (2011) kama Ebun

Ifedolapo (2015) kama muuguzi Titi

Aromimawe (2016) kama Iya Feranmi

Ireje (2016) kama Mrs Folawiyo

Gangan (2016) kama Radeke

Full House (2016) kama Mama

Omo Emi (2017) kama Mummy Funmi

Question Unanswered (2017) kama Mrs Clara

Jail (2017) kama Agatha

Tiwa's Baggage (2017) kama Iyabo

Ile Wa (2018) kama Mama Kate (pia aliandika na kuongoza)

Dirty Dirtier (2018) kama Mrs Shola

Adebimpe Omo Oba (2019) kama Olori

Apeka (2021) kama Mama Sinaayomi

Mimi's Voice (2021) kama Mrs Adetunji (also director)

Eyan Ni Mi (2021) kama Mama Twins

Onika (2022) kama Fadesewa

Cookie Spot (2022) kama Efe

Murder at the Bar (2022) kama Kebe

Third Eye (2022) kama Evelyn (also director)

Badcop (2023) kama Madam Nadia

Shattered Innocence (2023) kama Mummy Dele

Ibro Ijaya (2025) kama Iya Bose

Àdùnní: Ògìdán Bìnrin (2025)kama Sister Bola


No comments