Amani ikistawi, Takwimu zinaongea; Amani ikitoweka, Takwimu zinalia
Kuna usemi usemao "namba hazidanganyi." Lakini ukweli usiopingika ni kwamba namba hizi hazitokei kwenye ombwe; zinahitaji mazingira tulivu ili kukua, kushamiri na hatimaye kutoa tafsiri ya maisha bora kwa mwananchi.
Tanzania ya leo, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inashuhudia mapinduzi makubwa ya takwimu katika sekta za kijamii na kiuchumi. Mapinduzi haya si bahati mbaya, bali ni matokeo ya moja kwa moja ya amani na utulivu wa kisiasa ambao taifa letu limeendelea kuukumbatia.
Kutoka Miaka 51 hadi 68: Ushindi wa Uhai
Tukitazama takwimu za wastani wa umri wa kuishi, kuna jambo la kujivunia. Mwaka 2000, wastani wa umri wa Mtanzania kuishi ulikuwa miaka 51 pekee. Leo, takwimu zinaonyesha tumefikia wastani wa miaka 68. Ongezeko hili la miaka 17 ni ushahidi wa kuimarika kwa huduma za afya na lishe.
Lakini tujiulize, katika nchi zenye machafuko, namba hizi zinasomekaje? Jibu ni rahisi: Takwimu zinalia. Vita na vurugu hupunguza umri wa kuishi, hubomoa hospitali na kukimbiza madaktari bingwa. Amani yetu imetuwezesha kujenga taasisi kama JKCI na MOI ambazo leo hii zinatoa tiba bobezi na kupunguza rufaa za nje ya nchi.
Maji na Elimu: Mapinduzi ya Haki na Utu
Haki ya mwananchi kupata maji safi na elimu bora ndio msingi wa ustawi. Takwimu zinaonyesha uandikishaji wa watoto shule za msingi umefikia asilimia 98 mwaka 2024. Huku upatikanaji wa maji vijijini ukipaa kutoka asilimia 32 mwaka 2000 hadi asilimia 79.9 hivi sasa.
Namba hizi ni "sauti" ya amani. Mtoto hawezi kwenda shule, na mwanamke hawezi kwenda kutafuta maji ikiwa kuna milio ya risasi mitaani. Amani imekuwa kama miundombinu isiyoonekana inayobeba miradi hii ya maji na madarasa ya ghorofa tunayoyaona leo.
Uchumi wa Viwanda na Mauzo ya Nje Katika nyanja ya uchumi
Tanzania imepiga hatua kutoka kuuza malighafi pekee hadi kuuza bidhaa za viwandani. Mauzo yetu nje ya nchi yameongezeka kutoka dola milioni 43.1 mwaka 2000 hadi kufikia dola bilioni 1.4 mwaka 2024.
Hii ni ishara kuwa wawekezaji wana imani na ardhi yetu. Kama Rais Samia alivyowahi kusema, "Amani ndio sumaku ya uwekezaji." Hakuna mfanyabiashara atakayeweka bilioni zake kwenye nchi ambayo hajui kesho yake. Ongezeko la mauzo haya ni sauti ya mashine za viwandani zinazofanya kazi kwa sababu kuna utulivu.
Wajibu wa Kila Mtanzania
Tunapojivunia mafanikio haya ya Serikali ya Awamu ya Sita, hatuna budi kukumbuka kuwa takwimu hizi zinaweza "kulia" na kuporomoka muda wowote ikiwa tutaruhusu amani yetu ichezewe.
Maendeleo ya watu, uchumi jumuishi, na ustawi wa kijamii tuliofikia ni matokeo ya mshikamano wetu. Tukilinda amani, takwimu zitaendelea kuongea lugha ya mafanikio. Tukichezea amani, takwimu zitashuka na kuanza kumlilia kila Mtanzania, kuanzia mjini hadi kijijini.
Kwa hakika, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imethibitisha kuwa amani ndio mtaji mkuu. Ni wajibu wetu sote kuuenzi mtaji huu ili vizazi vijavyo vikute takwimu zinazozungumza lugha ya utajiri na heshima

Post a Comment