RAIS SAMIA AWAKARIBISHA IKULU TAIFA STARS KWA CHAKULA CHA MCHANA



RAIS Samia Suluhu Hassan amewaalika wachezaji na benchi la ufundi la timu ya Taifa, Taifa Stars, kwa chakula cha mchana Ikulu, Januari 10, 2026. Mwaliko huo ni ishara ya kutambua mchango wao na heshima waliyoipa nchi baada ya kufuzu hatua ya 16 bora katika michuano ya AFCON 2025 nchini Morocco.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, wakati wa mapokezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam. Timu hiyo imerejea nchini ikitokea Rabat, Morocco kwa kutumia ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyotolewa na Rais Samia.



Profesa Kabudi amesema kuwa kutokana na kiwango kilichooneshwa, Tanzania sasa imeingia rasmi katika orodha ya timu washindani barani Afrika na si washiriki pekee. 

Alisema wachezaji wameonesha kiwango cha juu cha ushindani, nidhamu na kujitoa kwa hali ya juu na kulipa heshima kubwa taifa barani Afrika. 

“Taifa Stars wameonesha umahiri wa hali ya juu na kujitoa kwa hali yao yote. Kwa mafanikio haya, Tanzania sasa si mshiriki tu wa AFCON, bali ni mshindani wa kweli,” alisema Profesa Kabudi.

Amesema mafanikio hayo ni msingi imara kuelekea maandalizi ya AFCON 2027 itakayofanyika kwa pamoja nchini Tanzania, Kenya na Uganda.



“Rais ameniagiza nije niwapokee na nimshukuru kwa dhati kwa uwekezaji mkubwa alioufanya katika sekta ya michezo, ambao matunda yake yameanza kuonekana,” alisema Profesa Kabudi.

Amewashukuru wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kuipokea timu hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

"Amani ni msingi wa taifa letu. Taifa lolote linalothamini michezo hulinda amani, na Tanzania imeendelea kuwa mfano wa nchi inayokabiliana na changamoto zake kwa njia ya maridhiano,” alisisitiza.



Naye Kocha Mkuu wa Taifa Stars Miguel Gamondi alisema wachezaji walipambana kwa hali ya juu na wanastahili pongezi kubwa kutoka kwa Watanzania wote.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema mkoa huo unaungana na serikali kuwapongeza Taifa Stars kwa kazi kubwa waliyoifanya, huku akibainisha kuwa maandalizi ya AFCON 2027 yanaendelea kwa kasi.

“Tumejipanga kikamilifu. Tumetuma kikosi maalum kwenda nchini Morocco kujifunza namna bora ya uendeshaji wa mashindano haya. Amani ndiyo msingi wa kila jambo, na tunahakikisha amani ya Dar es Salaam inalindwa wakati wote,” alisema Chalamila.

Aliongeza kuwa mkoa huo, kwa kushirikiana na sekta binafsi, unaendelea kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa hoteli za nyota tano, huku akiahidi kuwa ifikapo 2027 hakutakuwa na barabara itakayofungwa wakati wa mashindano.




Mapokezi ya Taifa Stars yalipambwa na shamrashamra za kipekee zilizosheheni ladha ya sanaa na utamaduni wa Kitanzania. Vikundi vya ngoma za asili vilitumbuiza kwa madoido, vikicheza kwa ufundi wa hali ya juu huku sauti za ngoma na vigelegele vikitawala anga la uwanja huo, hali iliyoamsha ari na fahari ya kitaifa miongoni mwa mamia ya mashabiki waliojitokeza kuwapokea mashujaa hao.

Vituko vya sanaa na utamaduni viliwakilishwa vyema na vibunifu mbalimbali, ikiwemo uwepo wa wahusika waliovalia mavazi ya vikaragosi ya dubu wakubwa wa rangi za kijani, bluu na nyeusi, ambayo ni rangi za bendera ya taifa. Ubunifu huu uliwavutia watu wengi, hususan watoto na vijana, na kufanya mazingira ya uwanja wa ndege kuwa kama tamasha kubwa la kijamii lililojaa furaha na amani.



Wachezaji wa Taifa Stars walionekana wenye bashasha wakizungukwa na viongozi pamoja na mashabiki, huku wakisindikizwa kila hatua na umati uliokuwa ukiimba nyimbo za ushindi. Muingiliano huu wa sanaa, ngoma, na mavazi ya utamaduni ulionyesha jinsi michezo inavyoweza kuunganisha taifa na kutoa fursa kwa wasanii kuonyesha vipaji vyao katika matukio makubwa ya kihistoria kama hayo.



Katika mashindano hayo yaliyoanza Desemba 21 mwaka jana kwenye makundi Taifa Stars ilifungwa na Nigeria 2-1 katika mchezo wa kwanza na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Uganda na Tunisia.

Kwa kufika hatua ya 16 bora Taifa Stars imevuna Sh Bilioni 1.9 pia imepokea Sh milioni 300 kama zawadi ya kila goli, mechi dhidi ya Uganda Sh milioni 100 na mechi ya Tunisia sh milioni 200.

Taifa Stars imeshiriki kwa mara ya nne katika michuano ya AFCON tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957 ambapo ilishiriki mwaka 1980, 2019 na 2023 na safari hii wamevuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.


No comments