AFCON 2027: RAIS SAMIA ASISITIZA WACHEZAJI WAZAWA KUPEWA NAFASI

 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito wa kimkakati kwa wadau wa soka nchini kuhakikisha wachezaji wazawa wanapewa kipaumbele na nafasi zaidi ya kucheza, ili kuijenga timu ya Taifa (Taifa Stars) kuelekea michuano ya AFCON 2027.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo katika Ikulu ya Dar es Salaam, wakati wa hafla maalumu ya kuwapongeza wanamichezo walioiwakilisha nchi vyema kimataifa, hususan kikosi cha Taifa Stars kilichofika hatua ya 16 bora katika michuano ya AFCON 2025 iliyomalizika nchini Morocco.

Maandalizi ya AFCON 2027 (Pamoja)

Akielekeza macho yake kwenye michuano ya AFCON 2027 itakayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda, Rais Samia alisisitiza kuwa uzoefu wa wachezaji wa ndani ndio utakaokuwa nguzo ya mafanikio ya nchi.

“Nitoe rai kwa wadau wetu wa soka kuhakikisha wanawatumia zaidi wachezaji wetu wa ndani. Wacheze mechi nyingi zitakazoongeza viwango vyao na kuwapatia uzoefu utakaowasaidia kushindana kimataifa kwa faida ya Taifa Stars,” alisema Mhe. Rais.

Ili kufanikisha hili, Rais ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na TAMISEMI, kuongeza kasi ya kuibua vipaji vipya kuanzia ngazi za chini ili viweze kusaidia timu ya taifa katika fainali hizo zijazo.

Alisema kuelekea fainali hizo za mwaka 2027 kila Mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha tunakuwa na mshikamo wa kitaifa.



"Dakika 90" Dhidi ya Morocco

Rais Samia aligusia mchuano mkali wa hatua ya 16 bora ambapo Taifa Stars iliondolewa na wenyeji Morocco kwa kufungwa bao 1-0, mchezo uliogubikwa na utata baada ya Stars kunyimwa penalti ya wazi dakika za lala salama.

Mhe. Rais alifichua kuwa alifuatilia mchezo huo kwa hisia kali: “Kwa mara ya kwanza nilikaa kwenye televisheni kuangalia mechi ile dhidi ya Morocco mwanzo mpaka mwisho... Yale yaliyotokea yametokea kwa sababu wenzetu ni taifa lenye fedha na lenye ushawishi kwa waandaaji wa mashindano.”



Pongezi kwa Michezo Mingine

Mbali na soka, Rais Samia alitoa pongezi za dhati kwa wanamichezo wa riadha, ngumi, kriketi na futsal kwa mafanikio yao makubwa yaliyoendelea kulipeperusha vyema bendera ya Tanzania duniani. Alisisitiza kuwa jina la Tanzania sasa linasikika kwa heshima kubwa katika ulimwengu wa michezo, na akatoa mwito wa kuendeleza mshikamano wa kitaifa.

No comments