My Son, Barakatatu na Salim Ahmedy Issa watikisa orodha ya Tuzo za TAFFA 2025

 


WAKATI msimu wa nne wa Tuzo za Filamu Tanzania (TAFFA) ukitarajiwa kufikia kilele chake Februari 14, 2026 katika ukumbi wa Super Dome Masaki, uchambuzi wa orodha ya wateule unaonyesha ushindani mkali ambapo filamu za My Son na Barakatatu zimetajwa kutawala vipengele vingi zaidi.

Katika uchambuzi wa orodha hiyo iliyotangazwa jana, filamu ya My Son imejitokeza kama tishio kubwa ikiwa imetajwa kwenye takriban vipengele 12. Filamu hiyo inawania tuzo kubwa kuanzia Filamu Bora , Muongozaji Bora wa Kiume (Ramar King) , na Muswada Bora. Aidha, imetawala kategoria za ufundi zikiwemo sauti, mavazi, haiba, picha, na uhariri.

Filamu ya Barakatatu nayo imetoa kucha ikiwa inafuata kwa karibu na uteuzi katika vipengele takriban 10. Inachuana vikali na My Son katika kategoria ya Filamu Bora, Muswada Bora, na Muziki Bora. Pia imeng’ara katika vipengele vya picha, uhariri, na mandhari.

Kwa upande wa wasanii mmoja mmoja, Salim Ahmedy Issa ameweka rekodi ya kipekee msimu huu baada ya kutajwa kuwania tuzo katika kategoria tatu tofauti. Msanii huyo anawania tuzo ya Muigizaji Bora wa Kiume kupitia filamu ya Mwamwindi , Muigizaji Bora wa Kiume upande wa Tamthilia kupitia uhusika wa Dayo , na pia ametajwa kwenye kipengele cha Muigizaji Bora wa Kiume Chaguo la Watazamaji.

Kwenye upande wa Tamthilia (Series), Kombolela inaonekana kuwa na nguvu kubwa ikiwa imetajwa kwenye kategoria ya Tamthilia Bora pamoja na vipengele vingi vya ufundi na uigizaji. Inachuana na kazi nyingine kama Baraluko, Kiwembe, na Dosari ambazo pia zimepata nafasi kwenye kategoria mbalimbali.

Kategoria ya wasanii chipukizi (Upcoming) imewakutanisha damu changa kama Erick John, Mohamed Issa, na Tekla Adolf , huku ushindani wa kura za mashabiki ukiwakutanisha wakongwe kama Ernest Napoleon, Lumole Matovolwa, na Rachael Richard.

Tuzo hizi ambazo ziliahirishwa mwezi Desemba mwaka jana, sasa zinatarajiwa kutoa picha halisi ya ukuaji wa sekta ya filamu nchini ambapo jumla ya filamu 2,360 zilipokelewa msimu huu.Tuzo za TAFFA 2025 Kutolewa Februari 14 Super Dome Masaki

Tamasha na Tuzo za Filamu Tanzania (TAFFA) kwa mwaka 2025 sasa zinatarajiwa kutolewa rasmi tarehe 14 Februari, 2026, katika ukumbi wa kifahari wa Super Dome uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya ujio wa tuzo hizo, ambazo awali ziliahirishwa kutoka Desemba mwaka jana, imetolewa jana na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Gervas Kasiga, wakati akizungumza na waandishi wa habari. 



Dkt. Kasiga amebainisha kuwa usiku huo utakuwa kilele cha tamasha la mwaka 2025, ukihusisha ushindani katika kategori 26 pamoja na tuzo mbili za heshima.

Katika msimu huu, tuzo zimevutia ushiriki mkubwa wa kimataifa, jambo linaloashiria kukua kwa taswira ya sinema ya Tanzania nje ya mipaka. Dkt. Kasiga amefichua kuwa jumla ya filamu 2,360 zilipokelewa, ambapo kati ya hizo, filamu 239 pekee ndizo zinatoka Tanzania, huku nyingine zikitoka mataifa ya kigeni.

"Tuzo hizi ni ithibati itakayomwezesha mshindi kutanua soko lake la biashara na mauzo. Zinaonyesha umahiri na kutambulika kwa msanii," alisema Dkt. Kasiga, huku akiongeza kuwa suala la tuzo kuambatana na zawadi ya fedha (bahasha) atalifikisha katika mamlaka zinazohusika.

Licha ya mataifa ya kigeni kuingiza filamu nyingi, Dkt. Kasiga amewahimiza watayarishaji wa ndani kujikita katika kutengeneza masimulizi yanayochochea utamaduni wa Kitanzania. 

Tamasha la TAFFA 2025 halikuishia kwenye tuzo tu, bali liliendesha mafunzo ya uandishi wa skripti, utengenezaji wa sinema, na mbinu za kutafuta masoko na fedha katika warasha mbalimnbali zilizofanyika Agosti mwaka jana.



Katika hafla hiyo ya uzinduzi na utangazaji wa wateule (nominees), Rais wa Shirikisho la Filamu, Rajabu Amiry, ameiomba Serikali kuhakikisha washindi wanapata tuzo na zawadi za fedha taslimu ili kuinua thamani ya kazi zao. 

Mkurugenzi wa Studio19, Sam Janhpour, naye alipata nafasi ya kutangaza wasanii na kazi zilizofanikiwa kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho cha vipengele 26.

Kutangazwa kwa tarehe ya tuzo maana yake ni kuwa Mwaka huu tunahama kwenye mazoea kwani Tarehe 14 Februari, usiku wa mahaba utageuka kuwa usiku wa heshima na kifahari. Hii si sherehe tu, ni mapinduzi ya sekta ya filamu inayotengeneza ajira kuanzia teknolojia hadi masoko.

No comments