WAZIRI MKUU AIPONGEZA TAIFA STARS, AZITAKA TFF, ZFA KUFANYA MAPITIO YA KANUNI
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kuiwakilisha vyema nchi katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayoendelea nchini Morocco.
Pia, Waziri Mkuu ameyashauri mashirikisho ya mpira wa miguu ZFA na TFF yaangalie na kuzifanyia maboresho kanuni ili kutoa fursa zaidi kwa wachezaji wa ndani pamoja na kurefusha ligi ya Muungano.
"Wizara za Michezo pamoja na mashirikisho ya TFF na ZFA fanyeni kazi ya kuandaa timu, viongozi wetu wameandaa miundombinu twendeni tuandae timu ili watakapokuja tuwe tumejiandaa".
Moja ya maeneo ya kuandaa timu angalieni kanuni zenu yale mashindano ya Ligi Kuu, klabu bingwa, shirikisho la Afrika yatumie wachezi wote ila yanayoandaliwa na mashirikisho ya nchini angalieni kanuni mtumie wachezaji wazawa ili kutengeneza wigo mpana kwa wachezaji wetu.
Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo leo wakati akizindua Skuli ya Sekondari Chukwani, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Skuli hiyo imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.1 kwa lengo la kuwaandaa vijana wenye maarifa, ujuzi, ubunifu na maadili kwa kuunganisha nadharia na vitendo.
Akizungumzia mashindano ya AFCON, Waziri Mkuu alisema vijana wa Taifa Stars wameonesha ushindani na uzalendo mkubwa, na kusisitiza kuwa walipambana hadi mwisho.
“Vijana wetu hawakutoka mashindanoni, wametolewa mashindanoni. Kilichotokea hasa dakika za mwisho kimeonekana na Watanzania wote,” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa niaba ya Serikali, Waziri Mkuu amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi, mkuu wa msafara, Wizara husika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ZFA pamoja na taasisi zote zilizohusika katika maandalizi na ushiriki wa timu hiyo.
Akizungumzia maandalizi ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi waandaji, Waziri Mkuu alisema Serikali tayari imewekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya michezo chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi.
Alisema hatua inayofuata ni kuimarisha maandalizi ya timu kwa kupitia kanuni za mashindano ili kutoa nafasi pana kwa wachezaji wazawa kushiriki mashindano mengi, ikiwemo yale yanayoandaliwa na mashirikisho, pamoja na kuimarisha Ligi ya Muungano na ligi za mikoa.
Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mkuu aliwahimiza Watanzania kuendelea kuiunga mkono timu ya Taifa, akisisitiza kuwa AFCON 2027 itafanyika hapa nchini, hivyo mshikamano wa kitaifa na maandalizi ya mapema ni jambo la msingi.
Post a Comment