SERIKALI YASUKA MPANGO MPYA KULINDA HAKI ZA BINADAMU KATIKA BIASHARA NA UWEKEZAJI





Serikali imechukua hatua kubwa ya kuimarisha misingi ya utu na haki nchini kupitia mchakato wa kuhakiki rasimu ya Mpango Kazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu. Hatua hiyo inayotekelezwa kupitia Wizara ya Katiba na Sheria inalenga kuleta mapinduzi ya kiutendaji ambapo ukuaji wa uchumi utaenda sambamba na heshima na haki za msingi za kila raia.

Akifungua kikao kazi hicho mjini Dodoma kinachohusisha wadau kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Rwezimula, amebainisha kuwa mkakati huo ni kielelezo cha dhamira ya serikali kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi hayamuachi nyuma mwananchi wala kukandamiza utu wake.

Kukamilika kwa mpango huu kutaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza katika kuzingatia misingi ya kimataifa ya biashara na haki za binadamu. Hali hii inatarajiwa si tu kuboresha maisha ya wananchi bali pia kuongeza taswira chanya ya nchi katika medani za kimataifa, ikivutia uwekezaji wenye tija na unaoheshimu misingi ya kisheria na utu wa binadamu.

Dkt. Rwezimula amefafanua kuwa mpango huo umekuja wakati muafaka ili kuweka ulinzi wa kisheria katika kila hatua ya shughuli za kibiashara. Amesema lengo kuu ni kuhakikisha wafanyakazi katika sekta mbalimbali wanapata mazingira salama ya kazi, huku jamii inayozunguka maeneo ya uwekezaji ikilindwa dhidi ya aina yoyote ya unyanyasaji au ukiukwaji wa haki zao za msingi. Aidha, amesisitiza kuwa hifadhi ya mazingira ni kipaumbele kingine ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinanufaisha hata vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu, Nkasori Sarakikya, ameeleza kuwa serikali inatambua wajibu wake mkuu wa kuwa msimamizi na mlinzi wa haki za binadamu popote penye shughuli za kijamii na kiuchumi. Amebainisha kuwa mchakato huo unahusisha makazi na maeneo yote ambayo binadamu anafanya shughuli zake ili kuondoa mianya ya migogoro na dhuluma inayoweza kujitokeza.

Mchakato huu wa kuhakiki rasimu ya mpango kazi unatajwa na wachambuzi wa masuala ya kijamii kama hatua muhimu ya kurejesha utulivu na kuimarisha amani ya nchi. Kwa kuweka misingi imara ya haki katika sekta ya biashara, serikali inajenga daraja la kuaminika kati ya wawekezaji na wananchi wa kawaida, jambo ambalo ni nguzo kuu ya utengamano wa kitaifa.

No comments