RAIS SAMIA AFUNGUKA SABABU ZA KUMREJESHA PROF. KABUDI IKULU, ATAJA SIASA ZA DUNIA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi sababu ya kufanya mabadiliko ya mapema katika safu yake ya uongozi, akibainisha kuwa uteuzi wa Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), umechangiwa na uhitaji wa uzoefu wake kwenye medani za siasa za kimataifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwapongeza wanamichezo waliofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, Rais Samia amekiri kuwa mabadiliko hayo yamekuja mapema lakini ni ya kimkakati zaidi.

Uhitaji wa "Akili Iliyopevuka" Ikulu

Rais Samia ameeleza kuwa kutokana na kasi ya mabadiliko ya siasa za dunia, ambapo baadhi ya mataifa yanaitazama Tanzania kwa jicho chanya na mengine kwa jicho la changamoto, alihitaji msaidizi mwenye maarifa mapana.

“Ni too soon (mapema sana) kubadilisha lakini ni kwa sababu ya kuendana na siasa za dunia zinavyokwenda... Pale Ikulu nahitaji akili iliyopevuka yenye maarifa mapana na uzoefu mkubwa,” alisema Rais Samia.

Aliongeza kuwa Profesa Kabudi ni chaguo sahihi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujieleza na kufafanua mambo kwa kina, jambo ambalo litaongeza tija katika ofisi yake.

Ushirikiano wa "Vichwa Vikubwa"

Rais Samia pia amefafanua kuwa Profesa Kabudi atakuwa kiungo muhimu kati yake na jopo la washauri wapya aliojateua hivi karibuni, wakiwemo viongozi wastaafu wenye uzoefu mkubwa. Alitaja kuwa aliyekuwa Makamu wa Rais (Dkt. Philip Mpango) atamshauri masuala ya uchumi na miradi, huku aliyekuwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) akimshauri masuala ya jamii.

“Vile vichwa vikubwa vinahitaji mtu aliyetulia anayeweza kushughulika nao (to deal with them),” alisisitiza Mhe. Rais.

Mafanikio ya Utalii na Amani ya Nchi

Katika hatua nyingine, Rais Samia ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji kwa kuiwezesha Tanzania kutwaa tuzo tano za kimataifa, ikiwemo tuzo ya Tanzania kuwa nchi bora kwa utalii Afrika na duniani, pamoja na Zanzibar kutambuliwa kama kituo bora cha mikutano.

Mhe. Rais alihitimisha kwa kutoa onyo kwa wale wanaojaribu kuvuruga amani ya nchi ili kuchafua taswira ya Tanzania kimataifa:

“Kwa wale waliotaka kutuharibia amani ili kutuharibia sifa ya Tanzania washindwe na walegee. Tanzania itaendelea kuwa kitovu cha amani na haya tuliyoshinda tutaendelea kushinda miaka mingi mbele inayokuja.”


No comments