Shughuli za maisha zarejea, wito watolewa kwa wananchi kudumisha amani




"Sumu Haionjwi!" Huu ndio ujumbe mkuu unaoendelea kutolewa na wananchi mbalimbali nchini kote, huku wakirejea katika shughuli zao za kila siku kwa kasi, baada ya kumalizika sherehe za uhuru wa Tanganyika Desemba 9 wakiwa majumbani. 

Leo, Desemba 10, shughuli za kijamii na kiuchumi hasa sekta ya usafirishaji imeendelea kama kawaida, huku wito ukitolewa kwa kila mmoja kuhakikisha anaendelea kulinda amani na usalama wa taifa kwa kushirikiana na serikali.

Katika Kituo cha mabasi cha Msamvu, Morogoro, ambacho kinahudumia  barabara ya Dodoma, Iringa na Dar es salaam hali ya utulivu na uchangamfu imetawala.

Bilali Yasin mfanyakazi wa huduma za usafirishaji katika kituo hicho, ameeleza kuridhishwa kwake na hali ya amani nchini. "Nashukuru Serikali, kuna amani ya kutosha. Tunaendelea na kazi yetu ya kuhudumia wasafiri," alisema Yasin, akiongeza kuwa bado wako kazini na huduma za usafirishaji zinaendelea bila vikwazo. "Tunashukuru nchi kuwa na amani. Tunataka amani hii iendelee," alisisitiza.

Ibrahim, abiria aliyekuwa anaingia kwenye basi kuelekea Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kudhibiti vitisho vyovyote vya kiusalama. "Hali ni shwari (nzuri). Tishio la kiusalama linapokuwepo lazima lidhibitiwe. Tunaunga mkono namna serikali inavyodhibiti matukio haya," alisema Ibrahim, akionyesha imani yake katika jitihada za ulinzi na usalama nchini.

Taarifa kutoka TBC Morogoro zimeeleza kuwa shughuli zinaendelea kama kawaida Msamvu na wamehimiza wananchi "wasiogope, kila kitu kinaenda vyema."

Katika jiji la Dar es Salaam, shughuli za kibiashara na kijamii zimepamba moto, huku wananchi wakitekeleza majukumu yao bila wasiwasi. Kauli ya "Sumu haionjwi" inatumika kuwakumbusha watu kuacha matukio yaliyopita na kuendelea na maisha yao ya kawaida, kwani amani ni rasilimali muhimu ya taifa.

Oktoba 29 na Desemba 9 zinatajwa kama siku ambazo sasa zimepita, na umuhimu upo katika kuendeleza maisha ya kawaida.Abiria wanaweza kusafiri kwa uhuru kutoka kituo kimoja kwenda kingine, ishara tosha ya hali ya utulivu nchini.

Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi bega kwa bega na wananchi kuhakikisha amani inalindwa, na kwamba kila mmoja anaweza kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na usalama.

No comments