Amani ni Nguzo ya Maendeleo, Serikali Yapongezwa na Wananchi wa Manyara

 



Wananchi wa Mkoa wa Manyara wamepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha amani, utulivu, na usalama wa taifa, wakisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya ustawi wa jamii na maendeleo. Leo, shughuli za kibiashara na kijamii zimerejea kwa kasi, huku hofu yoyote iliyokuwepo kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani ikiondoka kabisa.

Wananchi waliozungumza na waandishi wa habari wamesema hatua za haraka na madhubuti za Serikali katika kudhibiti watu waliopanga kuhatarisha amani zimeleta faraja kubwa na kuendelea kujenga imani kwa wananchi.

Jabir Abdallah, mkazi wa Babati Mjini, ameeleza kuridhishwa kwake:"Kwakweli hapa Manyara shughuli zinaendelea kama kawaida. Ninaishukuru Serikali kwa kuhakikisha inalinda amani."

Abdallah ameongeza kuwa Watanzania wamekataa kabisa kuburuzwa au kuhamasishwa kufanya vurugu, akisisitiza kuwa amani ndio rasilimali pekee isiyo na mbadala kwa maendeleo ya taifa letu.

Katika maeneo ya mitaa ya nje ya Babati Mjini, wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wameripoti kufurahia hali ya utulivu, na wanaendelea na shughuli zao bila usumbufu wowote. Walikiri kwamba hapo awali walihofia kurudiwa kwa matukio ya vurugu, akirejelea tarehe iliyopita ya Oktoba 29, 2025, lakini leo hali imekuwa shwari kabisa na kila kitu kinaendelea kama kawaida.

Hali hii inathibitisha dhati ya Serikali ya kuhakikisha mazingira ya kufanyia kazi na kuishi yanabaki salama kwa ustawi wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa taifa kwa ujumla.

Kutokana na umuhimu wa amani, wito wenye nguvu umetolewa kwa makundi yote ya jamii kushiriki kikamilifu katika kuilinda. Ujumbe huu umewalenga hasa vijana na viongozi wa dini.

Kwa Vijana: "Tuchague busara, umoja na ustaarabu tunapotafuta 'HAKI' si hasira, wala kutumia vurugu. Nguvu za vijana ni za kujenga, si kubomoa." Vijana wametakiwa kutokuwa chombo cha kuchochewa na badala yake wawe walinzi wa utulivu.

Kwa Viongozi wa Dini: Mmetajwa kama taa na faraja. "Tunawaomba muendelee kuwa daraja la upatanisho, na si ukuta unaowatenganisha raia na viongozi wao... Taifa linawategemea kama nguzo ya maridhiano na busara."

Wananchi wa Manyara wameihimiza Serikali kuendelea kuimarisha hatua za kudhibiti viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani ili Tanzania iendelee kuwa nchi ya matumaini na utulivu.

No comments