MAFUNZO YA UKUZAJI UJUZI YALIVYOMNUFAISHA MSOMI SHAMBANI IKUNGI

 



Licha ya kuwa na shahada mkononi, Eliya Memba, mwalimu kitaaluma, alikataa kukaa na kusubiri ajira za ofisini ambazo zimekuwa adimu katika sekta binafsi na serikalini. Badala yake, aliamua kurejea shambani kwa lengo la kuitunza familia yake, akiamini kuwa kilimo kina fursa ya haraka ya kumnyanyua kiuchumi kuliko kuanzisha shule ya chekechea ambayo ingehitaji mtaji mkubwa na nguvu nyingi kuanza. 

Maamuzi yake hayo sasa yanaonekana kuzaa matunda baada ya kunufaika na programu ya mafunzo ya ukuzaji ujuzi yaliyoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) kwenye eneo la kilimo na usindikaji.

Katika ziara ya timu ya wataalamu kutoka ofisi hiyo ya Waziri Mkuu iliyoongozwa na Msemaji wake Mkuu, Revocatus Kasimba, nyumbani kwa Memba wilayani Ikungi, hali ya mafanikio imeanza kujidhihirisha. 

Memba ambaye anajishughulisha na kilimo cha alizeti, akiwa pia amewekeza katika ufugaji wa ng'ombe na kilimo cha vitunguu aliwaaeleza wataalamu hao jinsi mafunzo yalivyombadili na kwamba katika msimu huu  anaamini atavuna kiasi kikubwa cha alizeti baada ya kuachana na kilimo cha mazoea.

Katika shamba lake la ekari mbili la alizeti, mkulima huyo alieleza namna elimu kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ilivyobadilisha fikra zake na kumpa mbinu mpya za kisasa za kilimo hicho.

Kupitia mafunzo hayo, Memba na wakulima wenzake takribani 60 walifundishwa mbinu muhimu za kilimo cha kisasa ikiwemo upandaji kwa kutumia mistari, idadi ya mbegu katika mstari, nafasi, matumizi ya mbegu bora, mbinu za kuhimili maji (makinga maji) kwenye maeneo yenye mteremko, na muda sahihi wa kupanda. Alikiri kuwa hapo awali tangu amemaliza shahada yake ya ualimu na kuamua kuingia katika kilimo alikuwa anafanya kama wazazi wake walivyokuwa wakifanya.

Walikuwa wakulima wa mazoea, lakini elimu hiyo imempa matumaini makubwa ya kupata mavuno mengi msimu huu kuliko miaka ya nyuma, jambo litakalosaidia kuimarisha uchumi wake na wa Taifa kwa ujumla.

Mafunzo haya ya kukuza ujuzi yaliyotolewa mwezi Oktoba mwaka jana kwa wakulima wa wilaya ya Ikungi, yana lengo pana la kuongeza uzalishaji wa alizeti ili kuziba pengo la mafuta ya kupikia nchini. 

Kwa sasa, Serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kuagiza mafuta nje ya nchi, hatua ambayo inalenga kukomeshwa kwa kuwawezesha wakulima wadogo kulisha viwanda vya ndani. Hata hivyo, Memba alitoa wito kwa Serikali kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa urahisi zaidi na kuongeza nguvu katika kutoa mitaji ya kuendeleza zao hilo la kimkakati.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Ikungi, Bruno John Magazi, alieleza kuwa msimu huu unatoa matumaini makubwa kutokana na uwepo wa mvua za kutosha. Alisisitiza kuwa lengo la mafunzo hayo ya kukuza ujuzi yalikuwa ni kupanda mbegu ya kubadili namna kilimo hicho kinavyoendeshwa na jinsi ya kukamilisha mnyororo wake kwa manufaa ya wakulima.

Alisema mafunzo hayo hayakuishia kwa wakulima pekee, bali liliwahusisha pia wasindikaji wa zao hilo. Wasindikaji hao walipata elimu ya kuongeza thamani ya bidhaa zao kupitia ufungashaji bora na mbinu za masoko, hatua itakayowafanya kuwa washindani katika soko la ndani na nje ya nchi huku wakizalisha bidhaa safi kwa walaji.

No comments