DESEMBA10:Jeshi la Polisi Lasisitiza Amani, Laonya Kuhusu Maandamano Haramu
Jeshi la Polisi Tanzania, kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, limetangaza kuwa hali ya usalama nchini imeimarika na imeamka ikiwa shwari leo tarehe 10 Desemba 2025. Jeshi hilo limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kulinda maisha na mali zao, huku likisisitiza kuwa wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida.
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu ya Polisi, Dodoma, imefafanua kuwa hali hiyo ya usalama imedhibitiwa kufuatia ufuatiliaji wa karibu uliofanywa tangu jana tarehe 9 Desemba 2025 dhidi ya klabu za mitandaoni na njia nyingine zilizokuwa zikifanya mawasiliano kwa kupanga na kuhamasisha maandamano.
Jeshi la Polisi limeendelea kuwakumbusha wananchi kuwa hawapaswi kujitokeza kufanya maandamano yoyote leo tarehe 10 Desemba 2025 kwani yamepigwa marufuku tangu tarehe 5 Desemba 2025. Maandamano hayo yameelezwa kuwa haramu kwa sababu yamekosana na Sheria Mama, Katiba ya nchi ya mwaka 1977, na hasa Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura 322.
Jeshi la Polisi limewonya waasisi wa maandamano hayo, likisisitiza kuwa walikuwa wanahamasisha maandamano ya siku isiyo na kikomo dhidi ya amani, ikiwa ni miongoni mwa mbinu za kiuhalifu 13 walizokuwa wakizitumia kupitia mitandao.
Jeshi la Polisi limefafanua kuwa linafuatilia kwa karibu taarifa zote zilizotolewa tarehe 3 na 5 Desemba 2025 kuhusu wale waliohamasisha maandamano hayo kwa nia ya kukwamisha shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.
Taarifa hiyo inaonya kuwa, yeyote atakayejitokeza na kukataa kutii sheria za nchi kwa lengo la kuhatarisha usalama wa nchi na kusimamisha shughuli za kiuchumi na kijamii zisizoendelee, Jeshi la Polisi litamwadhibu. Jeshi la Polisi limetangaza kuwa litawadhibiti wale wote wanaohamasishana na kupandikiza mgawanyiko kwa kutumia udanganyifu, ili ibaki salama kwa Watanzania wema wote wanaopenda amani.
Wito kwa Wananchi
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za kila siku na kuzingatia maelekezo watakayokuwa wakipewa na Vyombo vya Ulinzi na Usalama popote walipo nchini.
Ujumbe mkuu unasisitiza kuwa: Hayo yote yanafanyika ili Taifa letu liendelee kuwa salama na sisi sote Watanzania wapenda amani tuendelee kuwa salama wakati wote.

Post a Comment