Mwankemwa akiwa pamoja na timu ya taifa |
DAKTARI Mkuu wa timu ya Taifa, ‘Taifa stars’ Mwanandi
Mwankemwa anatarajia kustaafu kuitumikia timu hiyo mara baada ya kumalizika
mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajiwa kesho jijini Nairobi, Kenya.
Akizungumza na Spoti Leo, wakati wa mazoezi ya Taifa stars
yaliyofanyika Karume jana, Mwankemwa alisema kuwa ameamua kustaafu kwa sababu
ya tatu, moja ni kuongezeka kwa majukumu, pili ni Mwenyekiti wa Chama cha
Madaktari pia mjumbe wa kamati ya tiba ambayo ipo chini ya shirikisho la soka
nchini (TFF).
“Kweli mimi nimeona ni busara kuachia majukumu kwa wengine
kwani nina majukumu mengi na mengine yananitaka nitoe maelekezo kwa
ninaowaongoza na ikumbukwe kuwa mimi pia nina ajira ambayo nahitajika
kuitumikia”, alisema Mwankemwa.
Pia alisema kuwa yeye alitarajia ule mchezo wa Taifa Stars na
Zimbabwe ndio ungekuwa wa mwisho kwake kuwepo kwenye benchi la Taifa stars ndio
maana alipiga picha na kikosi hicho lakini Kim Poulsen aliomba aendelee hadi
mashindano ya Chalenji yatakapomalizika.
Habari ambazo Spoti Leo imezipata nafasi ya Mwankemwa
itachukuliwa na daktari Cosmas Kapinga ambaye alikuwa dakatari wa timu ya Simba
kwa msimu uliopita.
Mwankemwa alisema alianza kujihusisha na tiba ya uanamichezo
mwaka 1982, baada ya kuumia goti na kushindwa kucheza mpira kwani alikuwa
akiichezea Ruvu stars na daadae alihamishiwa kikazi hospitali ya Temeke na
kuendelea kutibu timu za shule katika mashindano mbalimbali.
Mwaka 1984 hadi 1989 alikuwa anatibu timu za Redstars na
Panafrika, vilevile aliwahi kuwa daktari wa timu ya Vijana ya mkoa Dar es
Salaam ‘Mzizma United’.
Alianza kutibu Taifa Stars 2006, na anasema kuwa kocha mkuu
wa wakati huo Mshindo Msola ndiye aliyempendekeza enzi za FAT lakini alipokuja
kocha Marcio Maximo alishindwa kuwepo kwenye benchi la Ufundi la timu hiyo
kutokana na ajali ya gari aliyopata na kulazimika kupumzika kwa miaka miwili.
Baada ya kuja Jan Poulsen Mwanakemwa alirudi kuendelea
kuitumia Taifa stars hadi sasa ambapo ipo chini ya kocha Kim Poulsen.
Mwankemwa ambaye pia ni dakatari wa timu ya Azam vileviele ni
Mwenyekiti wa bodi ya olimpiki maalum.
Katika kazi yoyote kuna mafanikio, hivyo anajivunia
Kilimanjaro Stars ilipotwaa kombe la Afrika Mashariki na Kati akiwa na kocha
Jan Poulsen 2010 lakini pia nasema hatasahau kipindi timu ya Taifa ya Vijana
ilipogomea mchezo dhidi ya Nigeria wakiwa ugenini enzi za FAT na yeye
kuhusishwa na mgomo huo jambo ambalo anasema haikuwa kweli kwani wachezaji
walikuwa wanadai posho zao lakini uongozi wa akina Ndolanga kwa kuficha udhaifu
wao wakamsingizia yeye.
No comments:
Post a Comment