Waandaaaji wa mbio za mbuzi nchini wamesema jana kuwa mbuzi watakaoshiriki mbio hizo tayari wako kwenye kambi za mazoezi na kwamba zawadi za kuvutia zimeandaliwa kwa washindi wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo, Karen Stanley alisema kwa kwamba lengo la mbio hizo ni kukusanya Sh. bilioni moja kwa ajili ya kuchangia taasisi mbalimbali za hisani nchini.
Alisema tukio hilo la kifamilia la kila mwaka litafanyika Juni Mosi kwenye eneo la Green, mtaa wa Kenyatta, kuanzia saa sita mchana hadi saa 11.30 jioni ambapo gharama za tiketi zitakuwa ni Sh. 5,000 kwa watu wote na zitauzwa getini.
Mbio hizo za mbuzi za hisani zinafanyika kwa mara ya 13 mwaka huu tangu zilipoanzishwa mwaka 2001 na tayari zaidi ya Sh. milioni 660 zimeshakusanywa kwa ajili ya kuchangia mashirika na taasisi mbalimbali za kujitolea nchini.
Mwaka jana tukio hilo liliweka rekodi kwa kukusanya Sh. milioni 115 kwa ajili ya kuchangia mashirika 15, huku wahudhuriaji wakifika 4,200 waliolipa kiingilio getini.
Stanley alisema katika kuchangamsha siku hiyo wameandaa sehemu mahsusi kwa ajili ya aina mbalimbali za vyakula vya kuvutia kutoka sehemu maarufu zinazosifika kwa mapishi jijini Dar es Salaam.
“Pia tutakuwa na eneo lililokarabatiwa kwa ajili ya michezo ya watoto litakalowafanya watoto watakaofika kufurahi na kuikumbuka siku hiyo. Lipo eneo jingine jipya kwa watoto wadogo zaidi huku eneo jingine lililotayarishwa na Neverland Playgroup and Entertainment kwa ajili ya watoto wakubwa zaidi litakalokuwa na michezo kama sarakasi, ngoma, kucheza muziki na wachekeshaji kutoka asasi ya Kigamboni Community Centre,” alisema.
Miongoni mwa zawadi kubwa kwa mwaka huu ni tiketi ya kwenda Ulaya na kurudi, safari ya kwenda kwenye mbuga ya wanyama ya Selous na kifurushi cha kupata mtandao wa Intaneti kwa mwaka mzima ikiambatana na vifaa na uunganishaji.
No comments:
Post a Comment