H-BABA AMPUZISHA MAMA MZAZI MAKABURI YA NYASAKA
SIMANZI na majonzi vimetawala mtaa wa Nyasaka, wilayani Ilemela jijini Mwanza, wakati mamia ya wakazi, viongozi wa serikali, na wasanii walipojumuika kumpumzisha kwenye nyumba yake ya milele mama mzazi wa msanii nyota wa Bongo Fleva, Hamisi Ramadhan Baba maarufu kama H- Baba.
Mama huyo, ambaye alikuwa nguzo muhimu katika maisha ya msanii huyo, amepumzishwa leo Januari 12, 2026, baada ya mapambano ya muda mrefu na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa takribani miaka mitano.
Akizungumza kwa uchungu mbele ya waombolezaji, H-Baba ameeleza kuwa kifo cha mama yake ni pigo ambalo limeacha jeraha kubwa na la kudumu moyoni mwake. Alibainisha kuwa upendo usio na kifani alioupata kutoka kwa mama yake wakati wa uhai wake ndio uliokuwa unampa nguvu ya kupambana na changamoto za maisha.
"Kifo hiki kimeacha jeraha ambalo sitasahau maishani mwangu. Mama alikuwa kila kitu kwangu; upendo wake ulikuwa wa kipekee na ni pigo ambalo ni vigumu kuliziba," alisema msanii huyo kwa masikitiko akimalizia kwamba furaha yake ndio imeishia pale, hadhani kama kuna mtu atampa furaha.
Alisema waliishi maisha ya ufukara sana ndio maana aliacha starehe na kupambana kumuondoa mama yake katika nyumba ya udongo na kumjengea mahali pazuri pa kuishi yeye na bibi yake. Alisema bibi yake alipata shinikizo la kumuuguza mama yake na kufariki na tangu afariki bibi yake hali ya mama yake haikuwa nzuri aliendelea kupambana hadi alipofariki.
Akizungumza katika msiba huo pamoja na kutoa pole kwa wafiwa mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda aliwataka vijana kumuiga H baba kwa kuwa na nidhamu na anayeheshimu utamaduni. Amewataka vijana kuiga mtindo wa maisha wa H-Baba, hususan katika suala la kuheshimu wazazi, kuzingatia mila, na kuishi kwa maadili ya Kitanzania.
"Nawaasa vijana kuishi maisha yanayozingatia taratibu na maadili yetu. Igeni mfano wa H-Baba; pamoja na umaarufu wake, ameendelea kuwa kijana mwenye heshima na maadili kwa familia yake na jamii. Hili ni jambo la kupigiwa mfano," alisema Mhe. Mtanda.
Aliyekuwa mke wa msanii huyo, Flora Mvungi, naye alikuwepo kuungana na familia katika kipindi hiki kigumu. Akimzungumzia marehemu, Flora alisema mama huyo alikuwa mwalimu na mshauri mkubwa kwake, hasa katika masuala ya kulea na kutunza familia kwa upendo.
Naye msanii maarufu wa vichekesho, Brother K, alieleza kusikitishwa kwake na kifo hicho akisema: "Mama alikuwa na roho ya kipekee. Kila tulipomtembelea, alituonyesha upendo na kutujali kana kwamba sisi ni watoto wake wa kuwazaa. Tutamkumbuka kwa wema wake huo."
Mama wa H-Baba amepumzishwa, lakini mafunzo yake ya upendo na uvumilivu wa miaka mitano ya kuugua yataendelea kuishi kupitia watoto na ndugu aliowaacha.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.







Post a Comment