JE, UNAKWENDA KAZI NJE YA NCHI? NSSF YAKUHAKIKISHIA ‘BIMA YA MAISHA’ NA PENSHENI UKIREJEA NYUMBANI




MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umezindua mkakati maalum  unaolenga kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa vijana wa Kitanzania wanaopata fursa za ajira nje ya nchi (ughaibuni), ili kuwahakikishia usalama wa kipato, matibabu, na ustawi wa familia zao wanazoziacha nyumbani.

Kampeni hiyo inayokwenda sambamba na uimarishaji wa  "Hifadhi Scheme," inalenga kuhakikisha kuwa nguvu kazi ya Kitanzania inayotafuta maisha nje ya mipaka haipotezi uhusiano wake wa kiuchumi na kijamii na nchi yao, bali inatumia fursa hiyo kujenga uwekezaji wa kudumu.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa kuaga Vijana 109 wanaokwenda kufanya kazi ughaibuni hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo maalum ya kuwaaga vijana 109 waliopata ajira ughaibuni kupitia mawakala 15 wanaofanya kazi kwa karibu na Serikali, NSSF ilitumia nafasi hiyo kutoa elimu ya hifadhi ya jamii na umuhimu wa kujiunga na mfuko huo kabla ya kuvuka mipaka na kusajili vijana hao baada ya somo kukamilika.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Uhusiano wa NSSF, Lulu Mengele, alisisitiza kuwa kujiunga na hifadhi ya jamii ni silaha kubwa kwa kijana anayekwenda kufanya kazi mbali na nyumbani.

"Tunawataka vijana hawa wasiondoke hivi hivi. Kujiunga na NSSF kupitia Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Wananchi kutawawezesha kujiwekea akiba ambayo itawalinda dhidi ya majanga, kutoa bima ya matibabu kwa familia wanazoziacha, na muhimu zaidi, kuwa na uhakika wa maisha pindi mikataba yao itakapokamilika na kurejea nchini," alisema Mengele.

NSSF imebainisha kuwa mkakati huo unatekelezwa kupitia Hifadhi Scheme (National Social Security Scheme for Self Employed), ambayo imeanzishwa mahususi kuhudumia wananchi waliojiajiri na wale wenye mikataba ya vipindi maalum, unalenga pamoja na  makundi ya Vijana wanaofanya kazi nje ya nchi (migrant workers), wapi Wajasiriamali wadogo (Machinga na Mama Lishe), Sekta ya usafirishaji (Bodaboda) na Wakulima, wafugaji, na wasanii.

Kupitia skimu hii, mwanachama anaruhusiwa kuchangia kuanzia kiasi cha Sh 30,000 au 52,200 kwa mwezi, na anaweza kutekeleza mchango huo kidogo kidogo kwa siku, wiki, au msimu kupitia njia rahisi za kidijitali kama mfumo wa (ARAFA-USSD) *152*00#.

Meneja Mengele alifafanua kuwa kipato kinachopatikana nje kinapaswa kuwa chachu ya uwekezaji nchini. Kupitia NSSF, mwanachama anajihakikishia mafao ya uzazi, matibabu, ulemavu, na hata msaada wa mazishi. Aidha, skimu hiyo inatoa fursa ya kuchukua sehemu ya michango (mafao ya kujitoa) kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo hapa nyumbani.

 Ili kujiunga, kijana anahitaji tu kuwa na umri wa miaka 15 hadi 70 na kuwa na Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA). Huduma zote kuanzia usajili, ulipaji michango, hadi uhakiki wa salio zinafanyika kiganjani kupitia lango la huduma la NSSF (NSSF Portal) au mifumo ya ARAFA-USSD, jambo linalomrahisishia kijana aliyeko ughaibuni kusimamia akaunti yake akiwa popote duniani.

Mkakati huu wa NSSF unatajwa kama hatua kubwa ya kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kupunguza umaskini wa kipato na kukuza nguvu ya uzalishaji. Wakati nchi ikielekea 2026, amani na utulivu uliopo nchini unazidi kufungua milango ya ajira nje ya nchi, na NSSF sasa imesimama kama mlinda usalama wa kiuchumi wa vijana hao na familia zao.

No comments