RAIS SAMIA AANGAZIA UPATIKANAJI RAHISI NA NAFUU WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA BARANI AFRIKA
Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amesema mafanikio ya utekelezaji wa ajenda ya
nishati safi ya kupikia barani Afrika yanapaswa kupimwa kwa idadi ya kaya
zinazoweza kuipata na kumudu gharama zake.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo, tarehe 12
Novemba, 2026, katika Kikao cha Ngazi ya Juu cha Viongozi kuhusu Nishati Safi
ya Kupikia Barani Afrika, kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 31 wa Nchi
Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi
(COP31), jijini Antalya, Uturuki.
Amesema utekelezaji wa ahadi zilizotolewa
katika Mkutano wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika Paris mwaka 2024 umeanza
kuleta matokeo, akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ili nishati safi ya
kupikia izifikie kaya nyingi zaidi.
Akiwasilisha hatua za Tanzania, Rais Dkt.
Samia amesema upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini umeongezeka kutoka
asilimia 16 mwaka 2022 hadi asilimia 28.6 kufikia mwezi Machi 2026, ukitarajiwa
kufikia asilimia 35 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Ameeleza kuwa ongezeko hilo limechangiwa na
upanuzi wa huduma za umeme vijijini, ruzuku kwa vifaa vya gesi, na unafuu wa
kodi kwa teknolojia za kupikia. Hadi kufikia mwezi Machi, 2026, amesema Rais
Dkt. Samia, Serikali ilifanikisha usambazaji wa mitungi ya gesi zaidi ya
346,000 kwa ruzuku, majiko banifu zaidi ya 49,000 na majiko janja ya umeme
(induction cookers) zaidi ya 7,000.
Rais Dkt. Samia amesema Mkakati wa Taifa wa
Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unalenga kufikisha matumizi ya nishati hiyo
kwa asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034.
Akirejea matokeo ya programu ya CookFund, Rais
Dkt. Samia amesema programu hiyo imewezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia
kwa kaya zaidi ya 413,000 zenye takribani watu milioni 1.94 nchini.
Ameongeza kuwa programu hiyo imesaidia mamia
ya biashara za ndani na taasisi 45 za umma, zikiwemo shule, na kunufaisha
wanafunzi zaidi ya 62,000 nchini.
“Nishati safi ya kupikia ni uwekezaji katika maendeleo ya watu, uwezeshaji wa wanawake, fursa za kiuchumi na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,”amesema Rais Dkt. Samia.
Makamu wa Rais wa Uturuki, Mhe. Cevdet Yılmaz,
amesema jitihada za kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia barani
Afrika zinahitaji ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha na sekta
binafsi.
“Ni muhimu kupata fedha za kutekeleza mipango
hiyo. Ni muhimu pia kuhakikisha fedha hizo zinawafikia watu wanaozihitaji na
kuleta matokeo yanayoonekana,” amesema.
Aidha, ameishukuru Tanzania, hususan Rais Dkt.
Samia, kwa kuendeleza ushirikiano na wadau wa kimataifa kuhusu ajenda hiyo,
akieleza matumaini kuwa kikao hicho kitasaidia kuharakisha utekelezaji kwa
kuzingatia vipaumbele vya nchi za Afrika.
Akiongoza majadiliano hayo, Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), Dkt. Fatih Birol, amepongeza
hatua za Tanzania na mchango wa Rais Dkt. Samia katika kuendeleza ajenda ya
nishati safi ya kupikia barani Afrika.
Dkt. Birol amesema takribani dola za Marekani
milioni 740 kati ya dola bilioni 2.2 zilizoahidiwa katika mkutano wa Paris
tayari zimekwishaelekezwa katika miradi ya nishati safi ya kupikia barani
Afrika.
Katika hatua nyingine, Dkt. Birol amepongeza
jitihada za Rais Dkt. Samia kama kinara wa nishati safi ya kupikia barani
Afrika, akitaja mchango wake katika kutetea haki za wanawake, miongoni mwa
vipaumbele vya ajenda hiyo.
“Nilikutana na Mheshimiwa Rais (Samia) miaka
kadhaa iliyopita. Wakati huo, alikuwa akiongoza kikao kuhusu nishati safi ya
kupikia na usawa wa jinsia katika ajenda hiyo” amesema Dkt. Birol.
Kikao cha Ngazi ya Juu cha Viongozi kuhusu
Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika kimefanyika pembezoni mwa COP31,
kikihusisha mjadala wa viongozi na wadau wa namna ya kupanua matumizi ya
nishati safi ya kupikia katika kaya, shule na hospitali, na kusaidia biashara
zinazoongozwa na wanawake kupata ufadhili na masoko.




Post a Comment