TANZANIA KUWA MWENYEJI MAONESHO JUA KALI 2027
Na Mwandishi wetu, Kigali
Tanzania imepokea kijiti cha kuwa nchi mwenyeji wa Maonesho ya 27 ya Wajasiriamali Wadogo na Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Jua Kali yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2027.
Akizungumza baada ya makabidhiano ya bendera ya Afrika Mashariki baada ya uteuzi wa Tanzania kuratibu maonesho hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Alana Nchimbi, ameeleza utayari wa Serikali ya Tanzania katika kuandaa na kuratibu maonesho hayo kwa mwaka 2027.
"Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapokea kwa unyenyekevu na furaha kubwa nafasi hii ya kuwa nchi mwenyeji wa Maonesho ya 27 ya Wajasirimali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki," alisema.
Aidha ametoa shukrani kwa Sekretarieti ya EAC na nchi Wanachama kwa kuonesha imani kubwa na kuipa heshima Tanzania kuwa mwenyeji wa tukio hilo kubwa la kiuchumi kikanda.
Vilevile, ameahidi kuwa kuelekea maandalizi ya maonesho hayo ya 27 yatakayofanyika nchini Tanzania, Serikali itashirikiana kwa ukaribu wa hali ya juu na Sekretarieti ya EAC, serikali za nchi wanachama, sekta binafsi, pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha maonyesho hayo yanakuwa ya kihistoria na yenye tija kubwa kiuchumi kwa wadau wote
Post a Comment